mourinho kawa mtamu Man United





Si mbaya. Kwenye korido za Old Trafford kwa sasa linatajwa jina moja tu, Mourinho...Mourinho...Mourinho! Unajua kwa nini, mabosi wa timu hiyo kwa sasa wanafikiria kumbakiza kocha huyo Mreno hadi mwisho wa mkataba wake na ikiwezekana kumpa mkataba mwingine wa kuendelea kubaki kwenye timu yao kwa miaka 10 zaidi hasa baada ya kuibadili Man United.
Man United haikuwa ikionekana kuwa kwenye ubora wa kubeba ubingwa kutokana na kiwango chake cha mwanzoni mwa msimu, lakini Mourinho amebadili upepo wa timu hiyo na kinachomfanya akubalike zaidi ni jinsi alivyoweza kukikabili kipindi cha mpito bila kutetereka.
Ushindi kwenye mechi tatu mfululizo, umeirudisha timu hiyo kwenye mbio za kuwania nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na hilo limeongeza hadhi ya Mourinho. Mabosi wamefichua kwamba hawana haraka ya kufanya mazungumzo ya kumwongezea muda wa kubaki klabuni hapo hadi 2020, lakini wanachoamini kwamba sasa wamepata kocha sahihi wa kuvaa viatu vya Sir Alex Ferguson.
Kingine kinachowavutia mabosi wa Man United ni staili ya uchezaji ya timu hiyo ikiwa tofauti kabisa na ilivyokuwa kipindi cha David Moyes na Louis van Gaal na sasa mpango uliopo ni kumweka Mourinho kwenye mipango ya muda mrefu baada ya mkataba wake wa sasa kufikia mwisho.
Licha ya kwamba kwa sasa Man United imeachwa kwa pointi 13 na vinara Chelsea kwenye msimamo wa Ligi Kuu, pengo ambalo linahitaji mapambano makubwa sana kuliziba.
Man United pia ipo nje ya timu zinazofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa pengo la pointi nne, lakini mabosi wa timu hiyo akiwamo Mkurugenzi Mtendaji Mkuu, Ed Woodward na wamiliki, Familia ya Glazer wamefurahishwa na kazi ya Mourinho.
Hata kipindi ambacho Man United ilikuwa kwenye mwenendo mbaya kwenye miezi ya Oktoba na Novemba, ambapo walishinda mechi moja tu kati ya nane za ligi, mabosi wa Man United walikuwa wakifikiria zaidi mwisho wa msimu na wanaamini katika Mourinho kwamba ataijenga upya timu yao.
Man United imetumia Pauni 500 milioni kufanya usajili tangu Ferguson alipoondoka miaka mitatu iliyopita, imebainisha kwamba chini ya Mourinho itaendelea kutumia pesa kunasa wachezaji inaowahitaji ambao wataifanya Man United kurudi kwenye makali yake ya kuwa tishio duniani.
Man United imebeba taji moja tu tangu Ferguson astaafu, Kombe la FA msimu uliopita, lakini chini ya Mourinho inaamini njaa hiyo itakwisha.
Woodward amepanga kumpa muda wa kutosha Mourinho aendelee kufanya mambo yake Old Trafford na kwamba mataji yatarejea tu chini ya kocha huyo Mreno.
Kwa kuanzia Man United itamwongeza mwaka mmoja Mourinho hadi 2020 na hilo litafanyika mwishoni mwa msimu.

Related

michezo na burudani 4908352109489695516

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii