Kitu cha arusha kama kawa arusha

http://maisharaisi.blogspot.com/2017/03/kitu-cha-arusha-kama-kawa-arusha.html
Wanaiita “kitu cha Arusha”. Ndivyo bangi inayolimwa mkoani hapa inavyofahamika kwa watumiaji. Japo wataalamu wanasema bangi inayolimwa mikoa karibu yote inafafana, inayolimwa Arusha inadaiwa kuwa ni tofauti. Pengine ni kutokana na eneo ambalo inalimwa ndani ya Hifadhi ya Arusha (Anapa) ambako ardhi yake bado ni nzuri na biashara ya mmea huo ulioharamishwa inaendeshwa maeneo yaliyo chini ya Mlima Meru, mlima wa pili kwa urefu nchini baada ya Mlima Kilimanjaro. Bangi ni mmea ambao majani yake hukaushwa na baadaye kuwekwa katika vishungi mithili ya sigara tayari kwa kuvutwa. Katika baadhi ya maeneo, hata mbegu zake nazo husokotwa pamoja na majani yaliyokaushwa kwa ajili ya kuvutwa. Pia, kuna maeneo ambayo mmea huo ulikuwa ukitumika kama mboga na hasa mbegu zake. Bangi huweza kuota hata sehemu ambazo hazijalimwa na hata kwa wazalishaji huhangaika kupanda mbegu na mvua zinaposhuka huota bila ya wasiwasi tofauti na mazao mengine. Mimea hiyo imeshaingizwa katika orodha ya dawa haramu za kulevya duniani kutokana na athari wanazopata wavutaji. Ni kutokana na kuharamishwa huko, Serikali za nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiendesha operesheni kubwa ya kupambana na kilimo, biashara na matumizi yake. Lakini vita hiyo inaonekana haiwezi kuwa na mshindi mapema kutokana na wakulima, wauzaji, wasafirishaji na watumiaji wa bangi kuwa na mbinu nyingi za kuhakikisha mmea huo unaendelea kuwa sokoni. Na wakulima na wafanyabiashara wa Kisimiri ni sehemu ya watu wanaofanya vita dhidi ya biashara hiyo kuendelea kuwa ngumu kuidhibiti au kuiondoa kabisa. Kilimo cha bangi kinaendelea kwa nguvu katika eneo linalotenganisha Hifadhi ya Taifa ya Arusha na kijiji cha Kisimiri kilichopo wilayani Arumeru. Takwimu za Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa kipindi cha Januari hadi Februari mwaka huu, zinaonyesha kuna kesi 73 zinazohusu watu 136 waliokamatwa na jumla ya kilo 638 na gramu 591 za bangi. Mbali na bangi, takwimu hizo pia zinataja kesi 14 za watuhumiwa 56 wa dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye uzito wa gramu 389. Dawa hizo zimepelekwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuthibitishwa. Vilevile, kuna kesi 56 za watu 77 wanaotuhumiwa kuhusika na jumla ya kilo 114 na gramu 750 za mirungi mkoani Arusha. Mwaka jana, polisi ilikamata tani 26 za bangi katika kijiji hicho, kiwango ambacho kinaonekana kuwa kikubwa kuliko vyote katika miaka ya karibuni. Arusha ni kati ya mikoa sugu katika ulimaji wa bangi ikiwa pamoja na Tabora, Morogoro, Iringa, Mara, Rukwa, Ruvuma na Tanga. Sehemu kubwa ya bangi inayolimwa Tanzania, huuzwa nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Ethiopia na Sudan. Ikiwa na idadi ya watu takriban milioni 50, Tanzania inashika nafasi ya nne duniani kwa uzalishaji wa bangi. Wajerumani walileta bangi Kisimiri Kilimo cha bangi kinatajwa kukithiri katika kijiji cha Kisimiri Juu kinachopakana na hifadhi hiyo wilayani Arumeru ambacho kiko pembezoni mwa Mlima Meru. Taarifa zinataja sababu ya kukithiri kwa kilimo na biashara ya bangi katika eneo hilo ni kutokana na wageni kutoka Ujerumani ambao waliwekeza kwenye kilimo cha pareto na baadaye kupanda bangi tangu miaka ya 1950. Mwandishi wa gazeti hili alifika katika kijiji hicho kinachotajwa kuongoza kwa kilimo cha bangi mkoani Arusha na ili kupata habari vizuri alijitambulisha kuwa ni mfanyabiashara na hivyo kupata fursa ya kukutana na mmoja wa wafanyabiashara wa bangi kijijini hapo. Katika baa mojawapo kijijini hapo, mwandishi huyo alikutana na muuza bangi aliyejitambulisha kwa jina moja la Lazaro na kutaka kujua kama anaweza kupata mzigo wa kutosha wa dawa hizo haramu kwa ajili ya biashara. Mfanyabiashara huyo alijibu kuwa bangi ipo ya kutosha na imehifadhiwa katika maghala yaliyopo kwenye nyumba za wakazi. Baada ya mwandishi kumuuliza kama anaweza kupata walau debe moja, muuzaji huyo alisema hata kama angetaka magunia 100 yangepatikana. “Mzigo? Upo, unataka kiasi gani?” alihoji muuzaji huyo akionekana kuchukua tahadhari kubwa. Baada ya kuambiwa kiasi kinachotakiwa, alitoka nje na kwenda kujadiliana na wenzake, kisha akarudi. “Nimemuuliza mhusika anasema upo ila amenitahadharisha kuwa usije ukawa mpelelezi unataka utukamate. Mzigo upo mwingi,” alisema. Hata hivyo, mwandishi wetu alisema siku hiyo hakwenda kuchukua mzigo, bali kuangalia kwanza mazingira ya kununua na na kusafirisha. Muuzaji huyo alimhakikishia usalama wa kutosha katika usafirishaji. “Inategemea unataka kiasi gani, lakini tunauza kwa wingi,” alisema muuzaji huyo. Alipoulizwa kuhusu usalama wa usafirishaji, alisema: “Aaah! Haina shida. Mimi mbona nimepitisha mzigo wangu pale (Hifadhi ya Arusha) karibu gunia 100 hivi karibuni? Niliweka chini ya matenga ya nyanya. Askari walikagua nyanya tukapita bila wasiwasi.” “Ila Mara nyingi tukiwa na mzigo mkubwa huwa tunapita njia ya Oldonyo tunatokea Ngaramtoni. Siku ya kusafirisha mzigo vijana wanapita kusafisha kwanza njia kama kuna askari anapewa chake kabisa.” “Vijana wengi hapa wametajirika kwa bangi. Kama mtu anasafirisha gunia 100 na kila gunia anauza Sh400,000 anapata pesa nyingi. Wewe hata ukichukua gunia moja ukitengeneza misokoto yako unapata faida kubwa.” Lakini muuzaji huyo hakutaka kuonyesha sehemu yalipo mashamba ya bangi, akisema kwa wakati huo ilikuwa ni hatari. Kijana mwingine aliyejitambulisha kwa jina la James, alisema kiasi kikubwa cha bamgi inayolimwa kijijini hapo, huuzwa nchini Kenya. “Hapa soko kubwa liko Kenya kwa sababu kule hakuna ulinzi mkali. Wakati mwingine inapitishwa mpakani pale Namanga na kwenye mipaka isiyo rasmi,” alisema James. Aliongeza kuwa usafiri mkubwa unaotumiwa kupeleka bangi nchini Kenya ni wa punda. Mbali na kijiji cha Kisimiri Juu, vijiji vingine vinavyotajwa kulima bangi mkoani hapa ni Olikokola na Fungalaoni. Tanapa inasemaje? Akizungumzia kilimo cha bangi katika mpaka wa Hifadhi ya Arusha na kijiji cha Kisimiri, mkuu wa kitengo cha ulinziwa Anapa, Maria Kirombo alisema hiyo inatokana na hifadhi hiyo kukosa mpaka mahsusi, hivyo kusababisha wanavijiji kuingia na kufanya shughuli za kilimo ikiwemo bangi. “Tatizo hifadhi hii haina buffer zone kwa hiyo wananchi wanaweza kuingia. Kutokana na hali hiyo tumeshafanya operesheni kadhaa na sasa tumeweka kituo maalumu ambacho askari hulinda kwa zamu ili kukomesha kabisa kilimo hicho,” alisema Kirombo. Alitaja baadhi ya operesheni zilizofanywa tangu mwaka 2012 kuwa ni pamoja na iliyoshirikisha Jeshi la Polisi ambayo ilihusisha hifadhi hiyo na Chuo cha Uhifadhi cha Mweka. Nyingine ni iliyohusisha Jeshi la Polisi na nyingine iliyofanywa na Hifadhi ya Arusha. “Tumeweka kituo cha ulinzi karibu na Mlima Meru ambacho kiko karibu na kijiji cha Kisimiri Juu. Lakini kwa kuwa eneo lenyewe lina baridi kali, askari wetu hulinda kwa kupokezana kisha wanarudi hifadhini,” alisema. Alisema kutokana na operesheni hizo, wananchi wa vijiji vya Ngarenanyuki na Kisimiri Juu wameanza kulalamika kuwa mazao yao yanafyekwa kwa kuwa wengi hupanda bangi katikati ya mashamba ya mazao ya chakula. Akizungumzia mafanikio yaliyotokana na operesheni hizo, Kirombo alisema kwa sasa wanahakikisha hakuna mashamba ya bangi. Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto ya mpaka wa hifadhi na wanavijiji, jambo wanalolifanyia kazi kwa kuanza kupima upya. “Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alishaagiza tuhakiki upya mipaka yetu na vijiji, kwa sababu kuna wakati mipaka ya vijiji iliingia hadi eneo la hifadhi na wananchi walikuwa wanaingia kulima,” alisema. “Kwa sasa kuna survey (uhakiki) inaendelea katika mipaka yetu na kijiji cha Kisimiri Juu. Tutakachofanya ni kushirikisha uongozi wa vijiji na kuweka makubaliano kulingana na vipimo vya GPS ili wasiingilie tena,” alisema Kirombo. Kirombo alisema ukaguzi unaofanywa katika hifadhi hiyo ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ili kupambana na dawa za kulevya na ujangili. Katika hifadhi hiyo, ulinzi unaonekana kuimarishwa kwa kila gari na pikipiki zinazoingia kupitia lango la barabara inayotoka Usa River, hutia saini na kisha askari hulikagua gari zima. Pia, utaratibu huo hufanyika katika geti la kutokea lililo umbali wa kilomita 24 kulekea Kata ya Ngarenanyuki. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema vita dhidi ya bangi inakwama kwa kukosekana ushirikiano kutoka kwa wadau wakiwemo maofisa kilimo na wenyeviti wa vijiji. DC Arumeru agoma kuzungumza Katika hali inayoashiria ugumu wa vita hiyo dhidi ya kilimo cha bangi, mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti alikataa kutoa ushirikiano kwa mwandishi wa habari hizi alipotafutwa kwa njia ya simu. Mnyeti ambaye amekuwa katika mgogoro na waandishi wa habari mkoani Arusha, alisema ameshatoa maelekezo kwa wenyeviti wa vijiji na asingependa kusikiliza waandishi wa habari. “Ninyi si mmeshagoma kuja kwenye vikao vyangu, unapiga simu ya nini? Nimeshatoa maelekezo kwa wenyeviti wa vijiji,” alisema Mnyeti na kukata simu. Hivi karibuni chama cha waandishi habari mkoani hapa kilimtangazia mgogoro Mnyeti baada ya kumkamata mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha ITV, Khalfan Liundi kwa madai ya kuandika habari za uchochezi. Akizungumza na viongozi wa Serikali za vijiji wilayani Arumeru, Mnyeti aliwataka kuwaadhibu watu wanaojifanya waandishi wa habari. “Wako wageni wanaoingia vijijini mwenu na ninyi hamjui wanafanya kazi gani. Wengine wanabeba makamera wakijifanya ni waandishi wa habari, wengine ni matapeli na wengine matapeli wanakuja kuchora ramani ili wapate habari ili majambazi wavamie vijiji vyenu,” alisema. “Vipo tu vyombo vya habari, kagazeti hata hakaeleweki tumekuwa ni kero kwa vijiji. Wako waandishi matapeli na ndiyo maana hata maendeleo hayapatikani vijijini. “Kila mtu amekuwa mwandishi wa habari, ukimuuliza ameishia darasa la ngapi, atakwambia la pili. Mimi nimeshawaambia hata waandike wachafue wanavyoweza, lazima tuchukue hatua.”