Waarabu sasa waitisha Yanga


Mashabiki wa Yanga watakuwa na kazi kazi moja
 Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga inaomba dua katika ratiba ya timu 32 bora za Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa leo, isipangwe na timu nane za kutoka Kaskazini mwa Afrika.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) leo litapanga ratiba ya mtoano ya mashindano ya Kombe la Shirikisho inayozikutanisha timu zilizotolewa katika Ligi ya Mabingwa dhidi ya zile zilizofuzu kwa hatua hiyo katika Kombe la Shirikisho mechi zitakazoanza kuchezwa Aprili 7 na 8 na marudiano Aprili 14 na 16.
Timu za Tanzania hususani Yanga, imekuwa na wakati mgumu wa kuziondoa timu za Kiarabu pindi zinapokutana nazo kwenye mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na CAF.
Katika kundi hilo la timu 16,  litatoa timu moja itakayokutana na Yanga kwenye hatua ya mwisho ya mtoano kabla ya ile ya makundi.
Timu kutoka mataifa ya kiarabu ni pamoja na MAS Fes na Ittihad Tanger (Morocco), CS Sfaxien na Club Africain (Tunisia), Mouloudia D’Alger na JS Kabylie (Algeria), Smouha (Misri) na El Hilal Elobied ya Sudan.
Siyo tu Yanga kwani hata Simba na Azam nazo mara kwa mara zimekuwa zikipokonywa tonge mdomoni na timu kutoka ukanda huo kila zinapobakiza hatua moja kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho.
Timu hizo nane kutoka ukanda wa Kaskazini mwa Afrika, zinaweza kuwa kikwazo kwa Yanga kuvuna utajiri wa Dola 275,000 (Sh 615 milioni) itakazozipata kwa kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga iliyoingia hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, italazimika kufunga na kuomba isikutane na moja kati ya timu hizo nane kutoka Uarabuni ili ijaribu bahati yake ya kufuzu hatua ya makundi.
Yanga iliyotolewa na Zanaco kwenye raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya 1-1 nyumbani na kulazimishwa suruhu ugenini Zambia.
Rekodi mbovu ya Yanga inajidhihirisha tangu mwaka 2000 hadi sasa ambapo timu hiyo imekutana na klabu za Uarabuni kwenye hatua ya mtoano mara saba na zote ikajikuta ikiondolewa ama kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho.
Mwaka 2007, Yanga ilitolewa na Esperance ya Tunisia kwenye raundi ya pili kwa jumla ya mabao 3-0 katika ligi ya mabingwa, ikaja kutolewa na Al Akhdar ya Libya mwaka uliofuata kwenye Kombe la Shirikisho kwa matokeo ya jumla ya mabao 2-1 ya raundi ya kwanza.
Mwaka 2009 ilitolewa tena na Al Ahly ya Misri kwa mabao 4-0 kwenye raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa, 2012 ikakutana na kichapo cha jumla cha mabao 2-1 kwenye hatua ya awali dhidi ya Zamalek ya Misri pia, kabla ya kutolewa kwa mikwaju ya penati 3-4 dhidi ya Al Ahly kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2014.
Mkosi huo uliendelea mwaka 2015 walipokwaa kisiki mbele ya Etoile Du Sahel ya Tunisia baada ya kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1 katika raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho na mwaka jana walijikuta wakiondoshwa na Al Ahly kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima alisema kuwa ingawa timu hiyo imekuwa na wakati mgumu dhidi ya timu za Kaskazini, bado anahisi kuwa inaweza kusumbuliwa hata na timu kutoka ukanda mwingine.
“Tuwe wakweli kuwa Yanga ya sasa haiko vizuri na kama kosa ilishafanya tangu mwanzoni kwa kusajili wachezaji wasioisaidia timu kutokana na kuwa na viwango vya kawaida.
Kwa jinsi soka la Afrika lilivyobadilika kwa sasa, ninadhani Yanga japo tunapenda kuona ikifanya vizuri, inatakiwa kujipanga hasa kwenye hiyo raundi inayofuata hata kama isipopangwa na Waarabu,” alisema Malima.
Nahodha wa zamani wa Yanga, kipa, Manyika Peter Manyika alisema kuwa timu yoyote ambayo Yanga watakutana nayo kwenye hatua ya mwisho ya mtoano ni ngumu na wanapaswa kujiandaa vizuri.
“Hakuna timu rahisi kwa sababu zote ambazo zimeingia hiyo hatua ni bora na ndio maana zimeweza kufuzu, hivyo Yanga inapaswa kujiandaa kikamilifu pasipo kujali inakutana na Waarabu au timu kutoka ukanda mwingine.
“Timu inapaswa kutafuta mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya timu nzuri hata moja ili wawe fiti zaidi, kwamba hata wakikutana na mpinzani mwenye makali namna gani, wasipate ugumu wa kupambana nao,” alisema Manyika.
Timu zilizofuzu 32 bora
Kombe la Shirikisho MC Alger, JS Kabylie (Algeria), Recreativo do Libolo (Angola), ASEC Mimosas (Ivory Coast), El Masry, Smouha (Misri), MAS Fes, Ittihad Tangier (Morocco), Rayon Sports (Rwanda), Hilal El Obeid (Sudan), Mbabane Swallows (Swaziland), Platinum Stars, Supersport United (Afrika Kusini), Club Africain, CS Sfaxien (Tunisia), Zesco United (Zambia)
Ligi ya Mabingwa
Yanga (Tanzania), KCCA (Uganda), RC Kadiogo (Burkina Faso), AC Leopards (Congo), AS Tanda (Ivory Coast), TP Mazembe (DR Congo), Gambia Ports Authority (Gambia), Horoya (Guinea), CNaPS (Madagascar), AS Port Louis (Mauritius), FUS Rabat, Wydad Athletic Club (Morocco), Ferroviario Beira (Msumbiji), Rivers United, Rangers (Nigeria), Bidvest (Afrika Kusini).

Related

michezo na burudani 566416655918532668

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii