Tanesco kufanya uchunguzi moto Aga khan

http://maisharaisi.blogspot.com/2018/02/tanesco-kufanya-uchunguzi-moto-aga-khan.html

Jengo lenye kituo cha Hospital ya Aga Khana Dodoma likiteketea juzi.Picha na Maktaba
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema litatuma timu ya usalama kufanya uchunguzi kuhusiana na chanzo cha moto katika Kituo cha Afya cha Aga Khan baada ya kudaiwa ulitokana na hitilafu ya umeme.
Moto huo ulitokea juzi katika kituo hicho na kusababisha sehemu ya kituo hicho kuteketea.
Akizungumza jana ofisa habari wa Tanesco Mkoa wa Dodoma, Innocent Lupenza alisema baada ya tume hiyo kumaliza kazi ya ukaguzi itaweka taarifa hiyo kimaandishi.
“Nimesikia watu wa zimamoto wanasema inawezekana tatizo likawa limesababishwa na umeme uliporudi katika jengo,” alisema Lupenza na kuongeza: “Tuna timu ya watu wa usalama watakwenda eneo la tukio leo (jana) kwenda kuangalia, wakiangalia wataweka hiyo taarifa kwenye maandishi.”
Akizungumzia tukio hilo juzi, ofisa utawala wa Kituo cha Aga Khan, George Washa alisema jengo lililoteketea lilikuwa likitoa huduma za X-ray na wagonjwa wa bima ya afya.
“Staff (wafanyakazi) wenzangu walikuja na kuniambia jengo la pili linaungua, nilichofanya ni kupiga simu zimamoto huku nikiwatoa wagonjwa nje na kuwaamuru waliopaki magari waondoke,”alisema.
Mmoja wa wagonjwa aliyekuwapo kwenye kituo hicho, Musa Jussi alisema moto huo ulianzia katika transfoma iliyopo nje ya kituo hicho.
“Nilipoona moto ikabidi nimbebe mwanangu na kukimbia nje ili kujiokoa, ila moto ulianza kwenye transfoma iliyopo katika jengo hili,” alisema.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Dodoma, Regina Kaombwe alisema chanzo cha moto huo ni kurudi kwa umeme ghafla ambao ulikuwa umekatika.
“Hili eneo umeme ulikuwa umekatika tangu asubuhi na uliporejea saa 10:00 jioni, jengo lilianza kuteketea,” alisema Kaombwe.
Alisema jengo hilo limeteketea lote na vitu vilivyokuwamo na kwamba, walifika eneo la tukio baada ya dakika 10 na hakuna kitu kilichookolewa.
Hata hivyo, Kaombwe alisema hakuna mtu aliyedhurika kwa kuwa wote waliokuwamo ndani walitolewa.
Naye kamanda wa polisi mkoani Dodoma, Gilles Muroto alisema tathmini ya hasara iliyopatikana inafanyika kwa kushirikisha vyombo mbalimbali.