Upelelezi bado kesi ya mhasibu ubalozini

http://maisharaisi.blogspot.com/2018/02/upelelezi-bado-kesi-ya-mhasibu-ubalozini.html

Upelelezi wa kesi ya utakatishaji dola 150,000 za Marekani inayomkabili mhasibu wa ubalozi wa Tanzania mjini Maputo nchini Msumbiji, Joyce Moshi haujakamilika.
Moshi (56), mkazi wa Temeke anakabiliwa na mashtaka tisa yakiwamo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, wizi akiwa mtumishi wa umma na utakatishaji wa fedha.
Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono ameeleza hayo leo Februari 27,2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema upelelezi haujakamilika na kwamba, wanasubiri nyaraka kutoka Msumbiji.
Mwanaamina ameiomba mahakama kesi ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.
Hakimu Shaidi ameutaka upande wa mashtaka kuendelea kufuatilia nyaraka ili upelelezi ukamilike. Ameiahirisha kesi hadi Machi 13,2018.
Mshtakiwa aliposomewa mashtaka alikana na yupo rumande kutokana na makosa yanayomkabili ya utakatishaji fedha kisheria hayana dhamana.