Adha na kero ya kuwa konda wa daladala Dar-1





Ni saa 11 alfajiri na tayari basi linalotoka Gongo la Mboto kuelekea Posta, limejaa abiria mpaka mlangoni. Munisi Elias ameshika lundo la fedha za sarafu anazozichekecha huku akipaza sauti yake kwa nguvu kuita abiria.
Wakati akiendelea kuwaita abiria, basi linaanza kukiacha kituo na kuelekea katikati ya barabara. Munisi anaingia ndani ya basi na mara moja anapaza sauti kuwapanga abiria akisema:
“Oyaa bi mkubwa, (mama) hebu kaa vizuri hapo, sogea mwisho ili na wenzako wasimame fresh.”
Hii ndiyo kazi ya utingo wa daladala maarufu kama makonda, ambayo huanza alfajiri na kumalizika saa tano au wakati mwingine hata saa sita za usiku.
Munisi anaendelea kuwapanga abiria huku akitoa kichwa nje mara kwa mara pindi basi linapofika kituoni ili kuwaita abiria.
“Kariakoo, Mnazi mmoja hiyo ya kuwahi,” anasikika.
Asubuhi hii abiria wapo kimya, kila mmoja akitafakari majukumu yaliyo mbele yake lakini kwa Munisi, yeye tayari ameanza kazi na kubwa analofanya ni kuhakikisha anawajaza abiria kadri atakavyoweza.
Ni kama basi hili halijai, wakati ukidhani limejaa ndivyo utakavyoona utingo akiongeza watu wawili katika kila kituo. Hapa kuna usemi maarufu wa utingo hawa kuwa ‘Daladala halijai’
Hali ndani ya basi hilo inaendelea kuwa si ya kufurahisha kutokana na msongamano wa watu, hakuna nafasi ya kukanyaga, waliosimama baadhi hawana mahali pa kujishika na wamesimama wakiwa wameshikilia viti.
Ubaya wa usafiri huu unazidi kuonekana katika kituo cha karibu na makutano ya Tazara, msongamano wa magari ni mkubwa na hapa basi linakaa kwa saa 1:15.
Wakati huo utingo anashuka na kuzungumza na utingo wa mabasi mengine, anavuta sigara kidogo na kuwatania madereva wa mabasi anaowafahamu.
Mara baada ya magari kuruhusiwa, Munisi anakimbia na kuingia kwenye gari, huku akipandisha suruali yake ambayo inamvuka, haina mkanda, haina zipu wala kifungo.
Hii ni sare ya bluu maalum kwa makonda wote. Lakini ya Munisi haifai kuitwa sare nadhifu bali unaweza kuiita nguo chakavu.
Kadhalika ndani ya suruali hiyo amevaa suruali ya dengrizi ya bluu na fulana. Juu ya fulana, amevaa koti ambalo ni sare na suruali nayo pia ni kuu kuu.
Tunapovuka mataa ya Tazara, Munisi anauliza, kama kuna mtu anashuka. Wanaitikia watu kadhaa ndani ya basi “Shushaa hapo Azam.”
Munisi anaonyesha kukerwa na anasema: “Watanzania bwana wanapenda raha kama maiti, sasa tumekaa kwenye foleni muda wote huo, si mngeshuka kule, pale mataa na hapa kuna umbali gani?”
Abiria mmoja anajibu:”Ingekuwa kuna abiria hapa usingesimama? We kazi yako kushusha, shusha tu,”
Munisi anamjibu: “Nenda zako mlevi wewe, usinitie nuksi asubuhi mie.”
Basi hilooo linaondoka na safari inaendelea kama kawaida hadi Mnazi Mmoja. Kabla hata abiria wanaoshuka hawajamalizika, tayari Munisi ameanza kupaza sauti yake akiwaita wapya.
Maisha ya makonda wa daladala ni tofauti na yale ya Mtanzania mwingine.
Aghalabu wao hulala kwa saa chache, kutumia muda mwingi wakiwa wamesimama, kupaza sauti kila mara kuita abiria na kingine ni kuishi katika msongamano ndani ya gari kila siku.
Wataalamu wa afya na saikolojia wanasema mfumo wa maisha ya watu wa kada hii umekuwa chanzo cha matatizo ya kiafya, msongo wa mawazo na hata baadhi wamebadilika na kuwa na tabia za ukorofi.
Dereva wa basi la abiria linalofanya safari zake kutoka Segerea hadi Kariakoo, Paulo Mwacha anasema kwamba kwa kawaida makonda na madereva wao hulala saa nne, tano au saa sita na huamka kati ya saa 10 au 11 alfajiri.
“Inategemea na mlichoingiza siku hiyo, siku ikiwa ngumu mnaendelea kufanya kazi ili mkamilishe hesabu ya tajiri (fedha anazotakiwa kupelekewa mwenye basi) na ikiwa nzuri mnalilaza gari mapema,” anasema.
Anasema mazingira ya makonda ni magumu kwa sababu ya kuwasiliana moja kwa moja na abiria na kusimama kwa muda mrefu.
“Kwa kawaida utingo hana siti kwenye gari, hata abiria akiingia anajua siti aliyokalia konda ni haki yake na hazungumzi bali humsimamia konda ili ampishe,” anasema.
Anasema ni kweli kuwa konda hutakiwa kuwaita abiria katika kila kituo jambo linalowafanya wapaze sauti kila wakati. Hata hivyo ‘wapiga debe’ walio katika kila kituo husaidia kazi hiyo kwa ujira wa Sh200 au 300.
Chuma Ulete
Utingo mwingine wa daladala, Ali Jumbe, anasema kazi yao ya kukusanya fedha wakati mwingine huwaingiza katika migogoro na abiria na imani za kishirikina
“Mtu anakupa Sh1,000 halafu wakati wa kudai chenji, anasema alikupa Sh5,000 hapo sasa unazuka ugomvi mkubwa,” anasema Jumbe
Pamoja na changamoto hiyo anasema kuna imani za kishirikina ambazo hutawala katika suala la kukusanya nauli.
Suala hilo ni chuma ulete, neno maarufu linalomaanisha wizi wa fedha kwa njia za kishirikina.
Jumbe anasema; “Unaweza kufanya kazi vizuri lakini jioni ukajikuta huna hela, una Sh 20,000. Kwa sababu kuna watu wana chuma ulete, wanakufanyia kiini macho, wanakupa nauli Sh 500 lakini unajikuta unawarudishia Sh 10,000 au zaidi.’
Jumbe anasema ili kujilinda na imani hizo, hutumia mfupa wa nguruwe na kuweka katika mfuko wa suruali.
Mtaalamu wa Saikolojia wa Chuo cha Sahare, Patandi, Tanga, Modesta Kimonga, anasema mazingira ya makonda wa daladala yanasababisha wawe na hasira na kuwa na akili yenye msongo wakati wote.
Anasema kitendo cha kupata muda mfupi wa kulala na kuwa kwenye vurugu muda wote kinasababisha wawe na hasira na hata kuongea lugha za kuudhi muda mwingi.



Related

kitaifa 2815787476661919302

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii