Mayanga amemwongeza mshambuliaji John Bocco, kwenye kikosi chake ambacho kitawakabili Zambia katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la COSAFA

https://maisharaisi.blogspot.com/2017/07/mayanga-amemwongeza-mshambuliaji-john.html
Bocco aitwa Stars kuimaliza Zambia COSAFA
Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Salum Mayanga,amemwongeza mshambuliaji John Bocco, kwenye kikosi chake ambacho kitawakabili Zambia katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la COSAFA, ikiwa ni siku mbili baada ya kuwatoa mabingwa watetezi Bafana Bafana.
Mayanga amemuita Bocco kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mbaraka Yusufu, ambaye hakucheza mechi dhidi ya Afrika kusini Bafana Bafana, kutokana na kusumbuliwa na hali ya hewa.
“Bado hatujamuondoa kikosini kumrudisha nyumbani lakini, tumeamua kumuita Bocco, kama ikitokea Yusufu kashindwa kabisa kucheza na pia ninataka kumtumia Bocco kwenye mechi ya kufuzu CHAN, dhidi ya Rwanda, “ amesema Mayanga.
Mayanga amesema anaamini Bocco ni mchezaji sahihi ambaye ataweza kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji kwani katika mchezo huo hatokuwa na Elias Maguli kwasababu yeye anacheza nje ya Tanzania.
Amesema kwa washambuliaji waliobaki nchini Bocco ni mtu sahihi na anaimani kubwa na mshambuliaji huyo ambaye amejiunga na Simba hivi karibuni.
Kocha huyo amesema hakumjumuisha mshambuliaji huyo kwenye kikosi chake cha awali kwakua alikuwa na matatizo yake binafsi na kumpa muda ili aweze kuyamaliza na kabla ya kumuita huko amezungumza naye na kumhakikishia yupo fiti kwa ajili ya kulipigania taifa lake.
Mechi ya kwanza ya kufuzu Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) dhidi ya Rwanda imepangwa kupigwa Julai 14 mjini Mwanza.