mungu ailaze roho ya marehemu maali pema peponi aamen.

http://maisharaisi.blogspot.com/2017/01/mungu-roho-ya-marehemu-maali-pema.html
UKUNGU wa simanzi umetanda kwa mara nyingine katika sekta ya michezo hususani, soka baada ya aliyekuwa kipa wa timu ya Ligi Kuu Bara, Kagera Sugar David Burhan kufariki akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Kipa huyo inaelezwa alianza kujisikia vibaya tangu wakielekea kwenye mechi yao ya Kombe la FA mjini Singida kukipiga na wenyeji wao Singida United, ambao waliowaondosha kwa mikwaju ya penalti.
Lakini, hali yake ilizidi kuwa mbaya kabla ya kuwahishwa jijini Mwanza ili kupatiwa matibabu katika hospitali ya Bugando na asubuhi ya juzi Mwenyezi Mungu aliichukua roho yake, ikiwa ni taarifa za ghafla kwa wadau wa soka nchini.
Ni kweli kifo kimeumbiwa viumbe hao, lakini kinauma namna kinavyokuja kwa ghafla bila ya watu kujiandaa kukipokea. Burhan ameondoka akiwa kijana mdogo na anayetegemewa katika soka la Tanzania. Inauma kweli, lakini kwa kutambua kuwa kifo ni siri ya Mungu, tunaungana na familia, ndugu, jamaa na wadau wote wa soka katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na kuwatakia kuwa na subira na uvumilivu.
Burhan keshakamilisha hesabu zake katika maisha ya duniani, waliosalia ni wajibu wetu kupata somo na kuzingatia kuwa, kifo huja ghafla na muhimu kujiandaa nacho.
Tunaamini Burhan alikuwa shujaa wa Kagera Sugar na soka la Tanzania kwa ujumla kwa sababu alikubali kusafiri umbali mrefu kutoka Kagera hadi Singida, licha ya kudaiwa alikuwa anajisikia vibaya. Alifanya hivyo kwa sababu tu alitaka kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa kwa klabu yake dhidi ya Singida United kwenye mchezo huo.
Kama asingekuwa shujaa angeweza kuugomea uongozi kuwa, hawezi kwenda kwa vile anajisikia kuumwa, lakini kwa moyo wa kiuanamichezo na uzalendo dhidi ya timu yake alifunga safari kabla ya hali kubadilika wakiwa safarini na hatimaye kufariki dunia.
Mungu amrehemu, lakini tukiendelea kukumbuka na kuuenzi mchango wake katika soka la Tanzania kwa klabu zote alizowahi kuzichezea zikiwemo Mbeya City, Majimaji ya Songea na nyingine. Tunamtakia kila la heri katika safari yake ya nyumba ya milele, tukimwambia buriani Burhan, tutakukumbuka na kuyaenzi uliyoyafanya kwenye soka la Tanzania.
»