Madiwani Dodoma wamkataa meya






Mgogoro kati ya madiwani na Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jaffar Mwanyemba umechukua sura mpya baada ya madiwani wa CCM kususia kikao wakishinikiza ajiuzulu wakimtuhumu kwa ubadhirifu wa Sh30 milioni za mradi wa maji wa Kata ya Zuzu.
Meya huyo pia anatuhumiwa kula rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Mwanyemba alisema asingeweza kuzungumza kwa kuwa alikuwa akiingia kwenye kikao cha ndani cha chama.
Awali, jana katika kikao cha madiwani wa CCM kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Manispaa ya Dodoma, chini ya Mwanyemba kuliibuka mvutano baada ya madiwani kumkataa.
Akizungumza baada ya kususia kikao hicho, Naibu Meya, Jumanne Ngede alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na meya kung’ang’ania kukiendesha licha ya madiwani kumkataa. Alisema madiwani walitaka kiendeshwe na katibu wao.
Alisema Februari 13, madiwani 43 walijiorodhesha na kusaini wakimpinga meya huyo na waliiwasilisha kwa mkurugenzi mtendaji kwa hatua zaidi.
“Tulifuata hatua hiyo ya kikanuni inayotutaka pale tunapokuwa na shaka tuwe huru kuhoji. Tuliwasilisha hoja tano ambazo tulimtuhumu meya kwa matumizi mabaya ya madaraka na matumizi mabaya ya fedha za mradi wa Zuzu,” alisema.
Ngede alisema wakati wakiendelea na hatua hizo, waliitwa na Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM ya Wilaya usiku kwa nyakati tofauti, jambo ambalo liliwalazimu kutoa taarifa kwa katibu wa CCM wa mkoa.
Naibu meya huyo ambaye pia ni Diwani wa Chamwino, alisema katibu wa CCM wa mkoa aliwataka kusubiri uamuzi wa chama hicho ngazi ya wilaya. Alisema suala hilo pia limelifikisha kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula.
Diwani wa Ipagala, Gombo Dotto alisema wamefikia hatua hiyo ili kupaza sauti zao... “Kuna kundi la madiwani wanaojiita wao ndiyo wenye halmashauri na lipo la waathirika ambao ndiyo wengi, hawajui halmashauri kunafanyika nini. Yapo mengi... ikafika hatua madiwani wakahoji.”
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Godwin Kunambi alisema baada ya kuanza kufuatilia sakata hilo, meya aliwasilisha hoja ya kutaka kumuondoa (mkurugenzi) lakini madiwani waliitupilia mbali baada ya kuonekana haina mashiko.
“Jana (juzi) madiwani walishawasilisha barua kulingana na kanuni za kudumu za manispaa na tayari nimeshamwandikia barua meya na kumkabidhi ili ajibu hoja za madiwani,” alisema.
Alisema kitakachofuata ni kupeleka suala hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kulingana na maelekezo ya kanuni.
“Nikishaandikiwa barua kanuni zinaelekeza nimtake meya ajibu tuhuma hizo ndani ya siku tano na mimi nitachukua majibu ya tuhuma na hoja za tuhuma na kuwasilisha kwa mkuu wa mkoa,” alisema.

Related

kitaifa 3653944426421761039

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii