Mwakyembe ahaidi kufatasheria.

http://maisharaisi.blogspot.com/2017/03/mwakyembe-ahaidi-kufatasheria.html
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na Katiba. “Tumeahidi mbele yako kwamba tutatenda kazi kwa nidhamu ya hali ya juu ili tukimaliza kipindi chetu cha awamu ya tano, Watanzania wajue tumetekeleza wajibu wetu ipasavyo,” alisema Dk Mwakyembe. Dk Mwakyembe aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli aliyemteua juzi kushika wadhifa huo. Viongozi wengine waliowateuliwa na kuapishwa jana ni pamoja na Profesa Palamagamba Kabudi, ambaye anakuwa Waziri wa Sheria na Katiba na Jaji Stella Mugasha (Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama). Wengine ni Job Masima (Balozi wa Israel), Sylvester Mabumba (Comorro), Dk Abdallah Possi (Ujerumani) na Alphayo Kidata ambaye anakuwa Katibu wa Ikulu Akizungumzia taarifa za mtandaoni kwamba alikataa uteuzi huo, Dk Mwakyembe alisema alishangazwa na taarifa hizo na kwamba, zimeandaliwa na watu waliojeruhiwa katika sakata la kashfa ya Richmond. Sakata hilo linahusu mkataba mbovu wa kuzalisha umeme wa dharura ambao Serikali iliingia mwaka 2006 na kampuni ya Marekani ya Richmond Development uliobainika baada ya kamati maalumu ya Bunge iliyoongozwa na Dk Mwakyembe kufanya uchunguzi. “Nilipata taarifa za uteuzi huu nikiwa naendesha kutoka Geita. Hizo taarifa za mitandaoni zinaenezwa na wale waliojeruhiwa katika (kashfa ya) Richmond. Ipo siku nitawasimulia yote, leo tuishie hapo,” alisema. Kuhusu ripoti ya kamati iliyoundwa na mtangulizi wake, Nape Nnauye kuhusu uvamizi wa studio za Clouds Media, Waziri Mwakyembe alisema atafuatilia ripoti hiyo kwa kutafuta taarifa za upande wa pili na kumshauri Rais Magufuli juu ya suala hilo. Balozi Possy alisema Ujerumani ni nchi yenye nguvu kiuchumi barani Ulaya, hivyo atatumia nafasi hiyo kuifungulia Tanzania fursa za uwekezaji na watalii. “Nafasi niliyopewa ni kubwa sana, nitajitahidi kuhakikisha kwamba Tanzania inanufaika na ukubwa wa Ujerumani kiuchumi. Nitahakikisha kupitia ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Ujerumani una kuwa na manufaa kwa Taifa letu,” alisema.