Yalio pelekea kutimuliwa hans pluijm haya hapa

MKURUGENZI wa Ufundi wa Yanga, Hans van der Pluijm, ametimuliwa katika nafasi hiyo, huku sababu za kuvuliwa cheo hicho zikitajwa. Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana, zinasema ukata ni moja ya sababu zilizochangia Yanga kufikia uamuzi wa kumtema Pluijm, uliofanywa na viongozi wa timu hiyo waliokutana kwa siri jijini, lengo likiwa ni kupunguza matumizi. “Jana kulifanyika kikao cha baadhi ya viongozi na kufikia uamuzi huo ambao umefanywa kwa maslahi ya pande zote mbili, yaani mwalimu na klabu,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye hakupenda jina lake kuwekwa hadharani, kwa madai kuwa hana mamlaka wa kulizungumzia hilo. Alisema kuwa, kuna mambo mengi yaliyochangia uamuzi huo, ikiwamo tabia zake, kwani kuna wakati ameonekana kuendekeza mambo madogo madogo. “Huwezi amini, hata posho kuna wakati huwa anashinikiza awe kwenye mgawo wakati hakupaswa kupewa, ukizingatia analipwa mshahara mkubwa zaidi ya mtu yeyote kwenye benchi la ufundi,” kilisema chanzo hicho. Lakini pia, inadaiwa kuwa Pluijm ameonekana kutoridhishwa na kitendo cha kuporwa nafasi yake na Kocha Mkuu George Lwandamina, hivyo kufanya mikakati ya chini kwa chini kuhakikisha mwenzake huyo anafeli. Chanzo cha kuaminika kinasema kuwa, Mholanzi huyo amewateka baadhi ya wachezaji ili kusambaza ‘sumu’ kwa wenzao, lengo likiwa ni kumharibia Lwandamina. Katika hilo, Pluijm anadaiwa kujifanya mtetezi wa wachezaji katika masuala mbalimbali, ikiwamo posho na nafasi ya kucheza, wengine wakiwa ni wale ambao yeye hakuwa akiwapa nafasi. Kati ya mbinu anazodaiwa kuzitumia Pluijm kumchafua Mzambia huyo ni kuwa karibu zaidi na wachezaji na kuzungumza nao kwa muda mrefu, lengo likiwa ni kuwafanya waamini yeye bado ni lulu Jangwani. Lakini pia, mwanzoni mwa mwaka huu, ilidaiwa kuwa Pluijm alishinikiza baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kugomea mazoezi, wakiushinikiza uongozi wa timu hiyo kuwalipa mishahara. Akiwa kama Mkurugenzi wa Ufundi, Pluijm amekuwa akionekana kutoshitushwa na matokeo mabaya wanayoipata timu hiyo kama ilivyojionesha katika mchezo wa Jumamosi iliyopita dhidi ya Simba, ambapo akiwa nje ya uwanja alionekana akitabasamu, huku akikataa kuhojiwa na waandishi wa habari.                                    

Related

michezo na burudani 6031049330741944853

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii