Ngassa kuifunga simba leo?

Kocha wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, akituma ujumbe kwa wachezaji wake, nyota wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, leo anaweza kuwapa bonge la zawadi mashabiki wa Jangwani pale atakapoivaa Simba akiwa na Mbeya City. Ngassa akiwa na kikosi cha Mbeya City, leo watamenyana na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Iwapo Ngassa ataisaidia timu yake hiyo kuichapa Simba leo, atakuwa ameisaidia mno Yanga kuelekea mbio za ubingwa wa ligi hiyo, hali ambayo ni wazi itapeleka furaha Jangwani. Watu wa Yanga kwa sasa wanaombea Simba iteleze katika mechi zake, ikiwamo ya leo, ili waweze kuwapiku kileleni mwa ligi hiyo na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kulibakiza kombe Jangwani. Katika msimamo wa ligi, Simba wanawazidi Yanga kwa pointi mbili, hivyo iwapo Wekundu wa Msimbazi hao watapoteza leo na wenzao kushinda kesho dhidi ya Mtibwa, ni wazi kuwa ubingwa unaweza kubaki Jangwani. Na kwa kiasi kikubwa, matumaini ya watu wa Yanga kwa Mbeya City kuisimamisha Simba leo yanabaki kwa Ngassa, ambaye ni mchezaji mzoefu mwenye kila aina ya mbinu za kimchezo. Wakati hayo yakiendelea, Lwandamina amesema kuwa ni ngumu kwa mchezaji kufikia malengo ikiwa atapuuzia suala la nidhamu. Kocha huyo alitoa ujumbe huo jana kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook. “Nidhamu na utii ndiyo siri ya mafanikio kwa kila mchezaji. Kuelewa na kufanya kazi yako kwa nidhamu ni muhimu katika kila mchezo, hasa kwenye wa soka, tena pindi kila timu inapokuwa na wachezaji 11… Ni vitu vichache (mbinu na juhudi) vinavyokusaidia kufanya kazi yako na kuleta tofauti kati ya kushinda na kupoteza mechi,” aliandika kocha huyo. Mzambia huyo aliongeza kuwa, ili mchezaji aweze kufanikiwa kimaisha au kitaaluma, lazima azingatie akili, hisia, tabia na vitendo chanya. Alisema kujiheshimu si kitu kipya, ni jambo ambalo limekuwa likizungumziwa miaka mingi, limekuwa likipewa sifa na watu waliofanikiwa. Lwandamina aliongeza: “(Mwanafalsafa) Aristotle aliwahi kusema: ‘Tabia njema ambayo huundwa wakati wa utoto ndiyo kila kitu’.” Lwandamina alitua Yanga mwishoni mwa mwaka jana kuchukua nafasi ya Hans van der Pluijm na kocha huyo alisaini mkataba wa miaka miwili.

Related

michezo na burudani 2636456284951749031

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii