Mbunge CCM nusura achapane na wabunge Chadema Dodoma




Mbunge wa Kiembe Samaki,  Ibrahim Raza
Mbunge wa Kiembe Samaki,  Ibrahim Raza (katikati) akiwatuliza Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Juliana Shonza (kushoto) na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea walipokuwa wakijibizana katika Viwanja vya Bunge, mjini Dodoma jana. 
 Wabunge wa Chadema jana walipambana kwa maneno na mbunge wa viti maalumu (CCM), Juliana Shonza, ambaye baadaye alienda polisi kuripoti sakata hilo.
Wabunge hao walidai Shonza aliwatukana kwa kuwaita wapumbavu baada ya kumwambia kuwa anachokifanya bungeni, hasa kuwasilisha mapendekezo ya adhabu dhidi ya wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) ni chuki binafsi ya kuondoka upinzani.
Mzozo huo ulizuka jana mara baada ya kikao cha mchana wakati wabunge wa Ukawa wakisubiri kukaguliwa kuingia jengo la utawala kwa ajili ya kikao chao na waandishi wa habari.
Shonza, ambaye aliwahi kuwa mwanachama wa Chadema, alikuwa akitoka jengo la utawala na kukuta wabunge hao wakisubiri ukaguzi.
Mbunge huyo alisikika akisema, “hamuwezi kunipangia cha kusema, kwa sababu hamkunileta bungeni,” huku akimfuata kwa karibu mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea. Sekunde chache baadaye, Shonza alisikika akisema “mnataka kunipiga” (huku akielekeza mkono kwa Suzan Kiwanga (mbunge wa Mlimba, Chadema), ambaye alisikika akimtaka Shonza amtaje aliyetaka kumpiga.
Baadaye wabunge wa upinzani walisikika wakihoji sababu za Shonza kuwatukana.
“Wengine hapa sisi ni mama zako,” alisikika Suzan Lyimo (viti maalum, Chadema).
Hata hivyo, baadaye wabunge wa CCM waliokuwa jirani walisogea na kumsihi Shonza kuachana na ugomvi huo, lakini mbunge huyo aliendelea kuwa eneo hilo, lakini baadaye walimchukua na kwenda naye jengo la Pius Msekwa.
Wakati wakiondoka naye, Pauline Gekul (Babati Mjini, Chadema), alimtaka Zainabu Vullu (viti Maalumu (CCM), kumfunda mbunge wao.
Alipoulizwa chanzo cha ugomvi huo, Kubenea alisema Shonza aliwatukana kwa kuwaita “wapumbavu” baada ya Joseph Selasini (Rombo, Chadema) kumwambia Shonza anachokifanya bungeni ni chuki.
Spika Job Ndugai alisema baadaye kuwa alipata taarifa za tukio hilo na kumshauri Shonza aliripoti polisi kwa kuwa ni la jinai na kwamba atawafikisha wabunge nane mbele ya Kamati ya Maadili kwa hatua zaidi.
Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa, Ernest Kimola alisema suala hilo limefunguliwa jalada la shambulio la kudhuru.
“Hatua inayofuata baada ya kuletwa kwa taarifa hii ni kuwatafuta wahusika ili tuweze kupata taarifa ya upande wa pili,” alisema Kamanda Kimola.

Related

kitaifa 6096449128945036135

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii