Kumbe! Mbao wateja wa Simba

http://maisharaisi.blogspot.com/2018/02/kumbe-mbao-wateja-wa-simba.html

Ah! Kumbe Mbao ni vibonde wa Simba bwana... Ndicho unachoweza kusema kutokana na rekodi baina ya timu hizo katika michezo mbalimbali tangu 2016.
Tangu 2016, timu hizo zimekutana mara 5, huku Simba ikishinda mechi nne ikipata sare moja tu dhidi ya Mbao mwanzoni mwa msimu huu.
Kipigo cha jana cha mabao 5-0, ilichokipata Mbao ni muendelezo wa uteja wake dhidi ya Simba.
Katika mechi tano Simba imefunga Mbao jumla ya mabao 12-5 pamoja na ushindani wote wanaonyesha vijana hao wa Mwanza.
Simba ilianza kuionea Mbao katika Ligi Kuu Oktoba 20, 2016 ikishinda 1-0 kabla ya mechi ya marudiano Aprili 10, 2017 kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 jijini Mwanza.
Katika fainali ya Kombe la FA iliyofanyika Mei 28,2017, Simba ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo kwa kuishinda 2-1 dhidi Mbao kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Mafanikio pekee ya Mbao walipata msimu huu baada ya kulazimisha sare 2-2 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Septemba 21, 2017, lakini katika mchezo wa marudiano uliofanyika Februari 26, 2018, kwenye Uwanja wa Taifa, Mbao ilikubali kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 5-0.
Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma alisema vijana wake walicheza vema hasa baada ya kufanya mabadiliko kipindi cha kwanza na kupata mabao mawili ya haraka yaliyowachanganya Mbao aliodai anawaheshimu kwa soka lao la ushindani.
"Tulikuwa na nia ya dhati ya kushinda tukiwa nyumbani ili kuzidi kujiweka pazuri kwenye mbio za ubingwa na tunashukuru tumepata matokeo mazuri," alisema Djuma, huku Nyoni akisema kazi yao ndio kwanza imeanza mpaka kieleweke.
Kocha Msaidizi wa Mbao, Ahmad Ally, alisema walicheza na timu kubwa na kuadhibiwa kwa makosa yao na matokeo hayo yamewaumiza kwani hawakutarajia kukutana na kipigo kikubwa cha aina hiyo.
"Simba wamekuwa wakitusumbua kila tunapokutana nao na tumeona makosa yetu na tunaendelea kurekebisha ili tufanye vema kwa mechi nyingine zijazo," alisema na beki kiraka wa Mbao, Boniface Maganga alisema wameumizwa na matokeo hayo.
VIKOSI
SIMBA: Manula, Kapombe, Kotei, Mlipili, Nyoni, Kwasi, Mkude, Ndemla/ Mzamiru, Kichuya, Gyan, Okwi/Mavugo.
MBAO:Iyvan, Maganga, Amos, Mwasa, Ndikumana, Njohole, Said, Lukindo, Sangija, Kyombo, Msuva/Kotecha, Mvuyekule/ Ismail
Rekodi zilivyo
LIGI KUU
Okt 20, 2016
Simba 1-0 Mbao
Apr 10, 2017
Mbao 2-3 Simba
Sept 21, 2017
Mbao 2-2 Simba
Feb 26, 2018
Simba 5-0 Mbao
KOMBE LA FA
Mei 28, 2017
Simba 2-1 Mbao