Pickford, kinda lililomng’oa mkongwe Hart England

http://maisharaisi.blogspot.com/2018/03/pickford-kinda-lililomngoa-mkongwe-hart.html

Jordan Pickford anatarajiwa kuwa kipa namba moja wa timu ya Taifa ya England katika fainali za Kombe la Dunia.
Fainali za Kombe la Dunia zimepangwa kuanza Juni, mwaka huu na England inatarajiwa kushiriki mashindano hayo.
Kinda huyo ameonyesha kiwango bora katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Uholanzi.
England ilishinda bao 1-0 mjini Amsterdam katika mchezo huo uliokuwa kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Mshambuliaji kinda wa Manchester United, Jesse Lingard alifunga bao hilo katika mchezo huo. England ilishinda bao 1-0.
Pickford mwenye miaka 24, anatarajiwa kurithi mikoba ya kipa nguli wa timu hiyo Joe Hart ambaye katika siku za karibuni amekuwa akishutumiwa kwa kiwango duni.
Wadau wa soka wamekuwa wakimtaja Hart kuwa ni mchezaji aliyechoka na anatakiwa kupata msaidizi makini.
Kocha wa England Gareth Southgate alimpa mikoba Pickford, baada ya kuvutiwa na kiwango chake katika kikosi cha Everton.
Katika mchezo huo, mchezaji huyo alicheza kwa kiwango bora na kumpa matumaini kwamba anaweza kusimama vyema katika milingoti mitatu kwenye fainali z Kombe la Dunia.
Mchezaji huyo anadaiwa kufuata nyayo za makipa wa zamani waliong’ara kina Peter Bonetti aliyetamba katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1970.
Pia kipa mwingine aliyetamba muda mrefu katika kikosi hicho David Seaman aliyeng’ara katika soka ya kimataifa duniani.
Katika mchezo dhidi ya Uholanzi, Pickford aliokoa michomo mingi ya washambuliaji wa timu hiyo waliokuwa na shauku ya kufunga mabao.
Hart mwenye miaka 30, alipoteza mwelekeo Manchester City baada ya ujio wa kocha Pep Guardiola, aliyemtoa kwa mkopo kwenda Torino ya Italia.
Hata hivyo, baada ya mkopo kumalizika, Guardiola alimpeleka katika klabu ya West Ham United kwa mkopo.
Southgate ameamua kuchukua uamuzi mgumu wa kwenda na Pickford akiwa ndiye chaguo la kwanza licha ya umri wake kuwa mdogo.
Pickford atakuwa kipa mwenye umri mdogo katika kikosi cha England kucheza Kombe la Dunia nyuma ya Paul Robinson (2006) na Ron Spingett (1962), walioshiriki fainalizo wakiwa na miaka 26 kila mmoja.