ATCL yajitosa kimataifa, kuuza tiketi duniani

http://maisharaisi.blogspot.com/2018/04/atcl-yajitosa-kimataifa-kuuza-tiketi.html

Mkurugenzi mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema juzi kuwa, wameamua kufikia makubaliano hayo kutokana na ukuaji wa huduma kupitia shirika hilo.
Alisema kwa vile Tanzania imeamua kufufua shirika hilo hawana budi kuendana na hali halisi ya uendeshaji wa mashirika ya ndege duniani.
Matindi alisema mkataba huo hautakuwa na madhara yoyote kwa pande zote na umepitiwa vyema na wanasheria wa Serikali.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, awali Tanzania kupitia shirika hilo iliingia hasara kutokana na kuingia makubaliano yasiyokuwa na tija, jambo ambalo alisema kwa sasa haliwezi kutokea.
“Mkataba huu tuliosaini leo (jana) hapa haujatuzuia pindi tukiamua kutoka tunaweza kutoka tu wakati wowote ule bila ya kipingamizi,” alisisitiza.
Pamoja na hayo alisema kupitia huduma hiyo, uuzaji huo wa tiketi utaisaidia ATCL kukua zaidi kimataifa.
Makamu wa Rais wa Shirika Hahn Air, Steve Knackstedt alisema wanaamini makubaliano hayo yataanza na taswira mpya katika ukuaji wa ATCL kwa kuwa kampuni yao ni kubwa na inatoa huduma hiyo karibu nchi zote duniani.