Real Madrid yapondwa kila kona Ulaya




Licha ya kupenya katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Frank Lampard amesema Real Madrid haina ubavu wa kuifunga Liverpool.
Lampard alisema Real Madrid haina kiwango cha kutisha kulinganisha na Liverpool na endapo timu hizo zitacheza fainali kocha Jurgen Klopp ataondoka uwanjani na kicheko.
Kauli ya nguli huyo wa zamani wa Chelsea na England, imekuja muda mfupi baada ya Real Madrid kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Bayern Munich ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Real Madrid inayonolewa na kocha Mfaransa Zinedine Zidane, ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.
Lampard, Rio Ferdinand na Steven Gerrard walisema Bayern Munich ilistahili kucheza fainali baada ya kuangalia kiwango cha Real Madrid katika mchezo wa juzi usiku.
“Bayern ilicheza kwa kiwango bora. Hii Real Madrid haipo vizuri kama ilivyokuwa miaka michache iliyopita,”alisema kiungo huyo wa kimataifa wa zamani wa England.
Gerrard aliyeipa Liverpool ubingwa wa Ulaya mwaka 2005 alisema Real Madrid haiwezi kutwaa taji hilo baada ya kuonyesha kiwango cha chini katika mechi zote mbili za nusu fainali.
“Ni fahari Real Madrid kucheza fainali mara tatu, lakini msimu huu haina ubora, Bayern ilistahili kusonga mbele katika mashindano haya,” alisema Gerrard.
Real Madrid inatarajiwa kumenyana na Liverpool au AS Roma katika mchezo wa fainali umepangwa kuchezwa Ukraine Mei 26.

Related

michezo na burudani 3123082290503734524

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii