rekodi mabao inavyoitesa Yanga kimataifa



Wakati Yanga inaondoka leo kwenda Algeria kuvaana na USM Alger katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini safu za ushambuliaji na ulinzi zina deni la kufuta rekodi isiyovutia ugenini kwenye mashindano ya kimataifa.
Katika mechi tano mfululizo za mwisho ambazo Yanga ilicheza ugenini kwenye mashindano ya ngazi ya klabu hivi karibuni, wawakilishi hao wamefunga bao moja tu huku wakishindwa kufunga mabao katika mechi tano.
Wakati washambuliaji wakionekana kuwa butu ugenini, safu ya ulinzi imekuwa na rekodi ya kuwa na wastani wa kuruhusu bao katika kila mechi katika michezo mitano iliyocheza ugenini.
Mechi pekee ambayo Yanga imefunga bao kati ya tano mfululizo za kimataifa ni ile dhidi ya St. Louis ya Shelisheli iliyochezwa Februari 21 Mjini Victoria ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Ukiondoa mchezo dhidi ya St, Louis, mechi nyingine nne za mwisho za kimataifa ambazo Yanga ilicheza ugenini kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, haikufanikiwa kuzigusa nyavu za timu pinzani.
Nuksi kwa Yanga kutofunga mabao ugenini ilianzia Machi 17, mwaka jana ilipotoka suluhu na Zanaco ya Zambia na kujikuta ikitolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sheria ya bao la ugenini, baada ya timu hizo mbili kufungana bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nchini.
Baada ya kutolewa kwenye mashindano hayo, Yanga iliangukia katika hatua ya mtoano ya mwisho Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilipangwa kucheza dhidi ya MC Alger kutoka Algeria.
Katika mchezo huo Yanga ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 nyumbani kabla ya kupoteza kwa kunyukwa mabao 4-0.
Ikionekana kama imefuta mkosi wa kutofunga bao ugenini baada ya kufumania nyavu katika mechi dhidi ya St. Louis iliyokuwa ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga iliendeleza ugonjwa katika raundi ya kwanza baada ya kutoka suluhu ugenini dhidi ya Township Rollers ya Botswana na kujikuta ikiondolewa kwenye mashindano baada ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani ilipofungwa mabao 2-1.
Kutolewa na Rollers kuliifanya Yanga idondokee kwenye hatua ya mtoano ya mwisho ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilipangwa kukutana na Waleytta Dicha ya Ethiopia.
Kwa mara nyingine, Yanga ilishindwa kufunga bao ugenini baada ya kulala bao 1-0 na Dicha, lakini ilifuzu hatua ya makundi kutokana na faida ya kushinda mabao 2-0 nyumbani.
Upande wa safu ya ulinzi ya Yanga, umeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita katika michezo mitano, ambayo kwa wastani ni kufungwa bao moja kwa kila mechi.
USM ina rekodi nzuri ya kufunga mabao kwa sababu katika mechi 10 za mwisho za mashindano ya kimataifa ilizocheza nyumbani, imefunga mabao 22 ambayo ni wastani wa mabao 2.2 kwa kila mechi lakini pia wamefungwa mara sita katika mechi zote 10 ambayo ni wastani wa bao 0.6.
Pondamali, Ulimboka walonga
Mchezaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema mbali na mbinu za nje ya uwanja, timu za kiarabu zina kiwango bora.
“Yanga ijipange ihakikishe timu yao iko fiti hata kucheza dakika 120 kocha ana wajibu wa kuangalia mfumo mzuri wa kuwapa matokeo, nadhani mashambulizi ya kushitukiza yatafaa,” alisema Mwakingwe.
Kocha wa makipa wa Yanga na kipa wa zamani wa Taifa Stars, Juma Pondamali alisema tofauti iliyopo na timu za kiarabu ni maandalizi.
“Kuna timu wachezaji wanaambiwa mkishinda mnapewa Dola 10,000, mkichukua kombe mnaongezewa Dola 10,000 unadhani kitakachotokea ni nini kama sio timu kupambana kufa na kupona, ndivyo wanavyofanya wenzetu,” alisema Pondamali.
Nyota wa zamani wa Taifa Stars, Adolph Rishard alisema mbinu itakayoivusha Yanga ni kucheza soka la kumiliki mpira.
“Sio mbinu ya kupaki basi.. la hasha! wajaribu kuiga Barcelona au Real Madrid soka lao wanalocheza, pia wawe na nidhamu ya hali ya juu katika mchezo,” alisema Rishard.
Alisema Waarabu wako mbali kwenye mbinu na ufundi wa mpira lakini akasisitiza kama Yanga ikijipanga na kuwa na nidhamu ya hali ya juu ya mchezo watafanya vizuri.
“Enzi zetu tuliwafunga Waarabu, sijui kizazi cha sasa kina nini, ila ninachokiona jamaa wanatushika kwenye nidhamu ya mchezo,” alisema Rishard.
Kipa wa zamani wa Simba, Mohammed Mwameja ameitaka Yanga kupambana kucheza kufa au kupona kupata matokeo ya sare, lakini isikubali kufungwa idadi ya mabao.

Related

michezo na burudani 3461273882450601643

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii