Kinondoni kubomoa makazi yote holela.

http://maisharaisi.blogspot.com/2016/12/kinondoni-kubomoa-makazi-yote-holela.html
Dar es Salaam. Manispaa ya Kinondoni itabomoa makazi yote holela yaliyomo katika eneo lake ndani ya miaka miwili kuanzia sasa na kuyajenga upya ikiwa ni moja ya mikakati yake ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta alisema kwa kuanzia wamepanga kuifumua Tandale na kuijenga kisasa, kwa mpangilio maalumu.
Lakini mchakato huo hautakuwa wa maumivu kwa wakazi wa maeneo hayo kwani Meya Sitta alisema kabla ya kuanza, watapima viwanja katika maeneo yote yasiyopimwa na baada ya taratibu kukamilika ndipo itakapotangazwa namna ya kuwaondoa.
Alisema wakazi watakaoondolewa watapewa chaguo la ama kuuza maeneo yao au kuingia makubaliano maalumu ya kupewa nafasi ya kuishi katika maghorofa yatakayojengwa.
Chaguo jingine ni kuwapa viwanja na fedha kidogo ili kuanzisha ujenzi wa kujitegemea au kujengewa nyumba nje ya eneo hilo.
Meya huyo ambaye pia ni mtoto wa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, marehemu Samuel Sitta alisema katika dunia ya sasa, ujenzi holela haukubaliki na kwamba mpango huo wa muda mrefu unatarajiwa kuanza mwaka 2018.
“Tandale hasa Uwanja wa Fisi ni moja ya eneo ambalo linatakiwa livunjwe kabisa na kujengwa nyumba za kisasa. Tukifanikiwa na hilo nina imani zile vurugu za Uwanja wa Fisi zitakwisha na kuruhusu shughuli za kimaendeleo.”
Sitta alisema ujenzi holela unaoendelea katika maeneo mengi nchini ni matokeo ya kutopanga miji mapema na si vizuri kuwahamisha wananchi katika maeneo waliyoko kabla ya kuwapangia pa kwenda.
“Ujenzi holela ni wa kusambaratika, lakini tukijenga maghorofa mawili ya kwenda juu zaidi tutaweza kuchukua wananchi wengi na pia manispaa itapendeza,” alisema Sitta.
Alifafanua kwamba mpango huo utachukua muda kidogo kwa sababu ni lazima waanze kuyapima maeneo holela ili kubainisha viwanja vitakavyotolewa kwa wakazi hao.
“Huwezi kumtoa mwananchi Tandale ukampa kiwanja Masaki kwa kuwa hataweza kumudu gharama za ujenzi badala yake atapelekwa maeneo kama Mabwepande ambako thamani ya ardhi ipo chini.
“Wale watakaoamua kubaki tutawatafutia maeneo ya kuishi kwa muda. Lakini hatuwezi kumjengea nyumba ya kawaida eneo hilohilo,” alisema.
Hata hivyo, Sitta alisema kwa mmiliki wa nyumba atakayeamua kubaki bila kuuza eneo lake, itamlazimu kujenga ghorofa ya kisasa ambayo itakuwa na maduka na sehemu ya makazi.
Sitta, ambaye alichaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni Oktoba baada ya Wilaya ya Kinondoni kumegwa na kuzaliwa ya Ubungo alisema ofisi yake pekee haitaweza kuendesha mradi huo, bali itashirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Tukiwa tayari na uthamini ukikamilika, tutaanza kufikia wawekezaji na wadau wa maendeleo walioko nje na ndani ya nchi.
“Tandale ina thamani na kuna barabara nzuri iliyojengwa kwa lami. Tukiweza kuwatoa hawa, tutajenga kitu kizuri na kuokoa maisha ya watu kutokana na halisi ilivyo katika eneo hili ambako kama mvua zikinyesha nyingi eneo hili hukumbwa na mafuriko,” alisema Sitta.
Alisisitiza kuwa mchakato huo, hauna lengo la kuwaonea wananchi, bali kuboresha maisha yao.
“Hakuna mtu anayependa kukaa katika maeneo holela.
Nitashangaa sana mtu anayefurahia kukaa maeneo holela wakati Kinondoni imepanga kuyaboresha.”
Alisema lengo ni kupima, kupanga na kuupendezesha mji na ifike kipindi wakazi waondokane na kuishi maeneo ambayo hayajapangwa ipasavyo ambayo hata kufikika ni shida.
Alieleza kuwa mchakato wa kupima viwanja utakuwa bure na utasimamiwa na manispaa ambayo ina wataalamu wa kutosha kwa shughuli hiyo.