Mgufuli akereka

http://maisharaisi.blogspot.com/2017/02/mgufuli-akereka.html

Rais John Magufuli
Rais John Magufuli amekerwa na utendaji wa vyombo vya haki na dola unaosababisha Serikali ipoteze mapato, kiasi cha kuamua kuweka bayana mambo aliyoyaita “magumu”, huku akitoa kauli ambazo zinaweza kuibua mjadala kuhusu mfumo wa utoaji haki.
Rais aliweka bayana mgogoro baina ya wateule wake wawili ambao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mashtaka; uzembe uliosababisha Sh7.5 trilioni zisichukuliwe na Serikali licha ya kushinda kesi za kodi; kesi kutomalizika mapema; Jeshi la Polisi na Takukuru kutofanya kazi zao vizuri; baadhi ya majaji kuendesha kesi ambazo mara nyingi Serikali hushindwa na udhaifu wa mawakili wa ofisi ya AG isipokuwa sita tu ambao alisema wanafanya kazi vizuri.
Rais pia alieleza kushangazwa na jinsi mahakimu 28 walioshtakiwa kwa makosa ya rushwa mwaka jana, lakini wote wakashinda kesi zao, jambo ambalo alisema linaibua maswali kuhusu utendaji kazi wa vyombo vya dola na utoaji haki za mahakama, huku akidokeza kuwa kuna majaji wengi walienda mapumzikoni nje ya nchi kwa kujigharimia, huku wanne tu kati yao wakilipiwa na Serikali.
Rais alisema hayo wakati akihutubia sherehe za kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria kwenye Uwanja wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.