Nchi 13 zabadilishana uzoefu wa elimu Dar

http://maisharaisi.blogspot.com/2017/02/nchi-13-zabadilishana-uzoefu-wa-elimu.html

Baadhi ya washiriki wa mkutano kuhusu elimu ulioshirikisha mawaziri wa elimu kutoka nchi 13, uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Picha kwa hisani ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
Hivi karibuni Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa mawaziri wa elimu kutoka nchi 13 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengineyo lengo la mkutano huu ulioratibiwa pia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni ( Unesco), llikuwa kujadili maendeleo endelevu ya Elimu 2030 (SDG4).
Pia, mkutano ulilenga kuainisha changamoto zinazofanana na kubadilishana uzoefu ili kuona namna changamoto hizo zinavyoweza kupatiwa ufumbuzi baina ya nchi washirika.
Tanzania yajipanga
Mwenyeji wa mkutano ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako Tanzania ipo tayari kuhakikisha inafikia lengo la nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu linalohusu elimu.
Ili kufikia azma hiyo anasema Serikali inajipanga kuhakikisha inatoa elimu yenye sifa tatu ambazo ni elimu bora, elimu inayojali usawa na elimu inayotengeneza fursa za kujiendeleza kwa wote.
Mkakati mwingine anautaja kuwa ni kuhakikisha elimu jumuishi na ile ya awali inatolewa shuleni pasipo malipo, sambamba na kuimarisha elimu ya msingi na sekondari kwa kuzifanya kuwa elimu ya lazima kwa wote.
‘’Ili mwanafunzi afanikiwe, tumebaini kuwa lazima msingi mzuri uwepo kuanzia elimu ya awali ambapo kimsingi huko ndiko mwanafunzi anatakiwa kujengwa na kujua kitu gani anatakiwa kuzingatia na kujifunza zaidi,’’ anasema Profesa Ndalichako.
Masuala tete ya kielimu
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako kuna masuala kadhaa yanayopaswa kufanyiwa kazi Tanzania na hata nchi waalikwa ikiwamo kuimarisha mifumo ya upimaji wanafunzi katika mchakato wa ujifunzaji. Anasema upimaji ndiyo nyenzo inayotumiwa na walimu kubaini kiwango cha uelewa kwa wanafunzi wake na nguvu anayopaswa kuongeza pindi anapobaini maeneo yenye changamoto.
Anasema ni muhali kwa mwalimu kujua maendeleo ya taaluma ya wanafunzi wake kama hakuwapima kwa njia mbalimbali ikiwamo kuwapa majaribio na mitihani.
“Upimaji kwa wanafunzi ndiyo njia pekee ambayo itamsaidia mwalimu kubaini kuwa wanafunzi wake wameelewa au hawajelewa na kama wameelewa basi lazima atajua wameelewa kwa kiwango gani ili hata anapotaka kuwaelewesha ajue atumie mbinu gani za kuwaelewesha,”anaeleza.
Alizungumzia pia kuhusu uimarishaji wa utoaji wa elimu kwa mtoto wa kike pamoja na watoto walio katika mazingira hatarishi. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa katika mkutano huo, kuna tofauti ya upatikanaji wa elimu kati ya watoto wa kike na wa kiume.
“Ili tuweze kufikia malengo ya elimu hadi mwaka 2030, lazima mwanafunzi wa kike apate elimu sawa na mtoto wa kiume, hivyo ni jukumu la wadau wote kuhakikisha malengo yanafikiwa,”anasisitiza.
Suala lingine liliorodheshwa kwenye majumuisho ya mawaziri, Profesa Ndalichalo anataja kuwa ni kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya stadi za kazi kuendana na soko la ajira.
‘’Ili kuweza kufikia uchumi wa kati, lazima mafunzo ya ufundi stadi yapewe kipaumbele, ili vijana wanapomaliza waweze kujiajiri wenyewe na siyo kusubiria kuajiriwa,’’ anaeleza na kuongeza: “Fani za ufundi zipo nyingi na endapo wanafunzi watafanya jitihada ya kutosha, tatizo la ajira kwa vijana litaisha kabisa. Kwa mfano, kuna ufundi seremala, ufundi wa magari, ufundi uashi, ufundi umeme, ufundi wa ujenzi. Vijana wakiamua kujikita huko ajira zitakuwepo na hiyo itatoa fursa kwa vijana kusaidia ukuaji wa uchumi na kuacha kukaa vijiweni.’’
Changamoto za elimu
Waziri Ndalichako anasema changamoto zinazoikabili elimu ya Tanzania ni pamoja na kuwapo kwa watoto wengi nje ya mfumo rasmi wa elimu, elimu kutowafikia watoto wenye mahitaji maalumu kwa usawa pamoja na kutokuwapo kwa mfumo wa elimu ulio endelevu hasa kwa wanafunzi wanaokatisha masomo kwa sababu mbalimbali.
“Tumekutana kila nchi ionyeshe ina mpango gani katika kufikia malengo hayo tutaangalia mipango inayofanana kati ya nchi na nchi pamoja na changamoto zake pia tutaangalia kama nchi tunakwendaje,” anasema.
Kauli ya Unesco
Mkurugenzi wa Unesco, Ann Ndong-Jatta anasema mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili vipaumbele vya kikanda na mapendekezo ya sera, kwa ajili ya tafsiri ya utekelezaji na ufuatiliaji wa ajenda ya elimu.
Alisema kila nchi imekuwa ikipitia changamoto mbalimbali za kielimu. Changamoto hizi zinatofautiana kulingana na mazingira ya nchi husika, hivyo lazima tuzijadili kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi.
“Tumekutana hapa kwa pamoja lakini kila mmoja wetu anazo changamoto ambazo zinamkabili katika nchi anayoiwakilisha, hivyo ni busara tukaainisha changamoto kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi ili hatimaye tufikie malengo ya elimu ambayo yameelekezwa kwa mataifa yote,”anasema Ndong- Jatta.
Mkutano huo uliofanyika kwa muda wa siku mbili ulishirikisha mawaziri kutoka nchi za Comoro, Djibout, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Madagascar,Mauritius, Rwanda, Shelisheli, Somalia, Sudan Kusini, Uganda na mwenyeji Tanzania.