Aggrey, Makapu, Mwinyi wabaki Stars



Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa ufafanuzi juu ya utaratibu utakaotumika baada ya Zanzibar kupata uanachama wa kudumu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Hivi karibuni CAF iliitambua Zanzibar kama mwanachama wa kudumu na sasa timu ya Taifa ya Zanzibar itaanza kushiriki mashindano yanayosimamiwa na CAF.
Akitolea ufafanuzi wa utaratibu huo, Katibu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema wachezaji waliowahi kuichezea timu ya Tanzania (Taifa Stars) hawataweza kuichezea timu ya taifa ya Zanzibar.
“Ipo hivi, kama mchezaji amezaliwa Zanzibar akaichezea timu ya taifa (Taifa Stars), ataendelea kuichezea timu hiyo.
“Lakini kama amezaliwa Zanzibar, lakini ameichezea timu ya vijana ya Tanzania huyo ataweza kuichezea Zanzibar Heroes na itakuwa hivyo hivyo kwa Bara,” alisema Mwesigwa.
Miongoni mwa wachezaji kutoka Zanzibar ambao wataendelea kuitumikia Taifa Stars ni Mwinyi Haji, Hamis Mcha, Said Makapu, Awadh Juma na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ambaye hata hivyo aliwahi kueleza kustaafu kuichezea timu ya taifa.
Akitolea ufafanuzi zaidi, Mwesigwa alisema hata hivyo taratibu zitakuwa zikibadilika taratibu kadri siku zinavyokwenda kulingana na muelekeo wa CAF na FIFA.
“Kwenye ligi, wachezaji kutoka Zanzibar ambao wanacheza Ligi Kuu Bara kama Cannavaro, hatakuwa na sababu ya kuombewa ITC kwa kuwa anacheza ligi ya ndani.
“Mfano mchezaji amezaliwa Zanzibar lakini anacheza Mbeya City, akataka kuhamia Toto African au Zimamoto, huyu haombewi ITC, kuna utaratibu unafanyika na anaendelea kucheza,” aliongeza Mwesigwa.
Kulikuwa na sintofahamu baada ya Zanzibar kupewa uanachama na kudhani kuwa katika eneo la michezo, Zanzibar sasa itakuwa na taratibu kama nchi nyingine hasa katika uhamisho wa wachezaji.

Related

michezo na burudani 2624358985719343847

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii