Kasi ya magufuli yaridhisha

http://maisharaisi.blogspot.com/2017/03/kasi-ya-magufuli-yaridhisha.html
Kabla hata ya kufikia mwaka mmoja na nusu katika utawala wake, Rais John Magufuli anatajwa kufanya mageuzi makubwa serikalini na ndani ya CCM, kasi ambayo inaelezwa kuwa ni ishara njema ya kuimarisha uchumi na nidhamu katika Taifa. Miongoni mwa mambo aliyoyafanya tangu alipoingia madarakani Oktoba 25, 2015, ni kuimarisha nidhamu na uwajibikaji serikalini ambako amekuwa akiwasimamisha kazi baadhi ya watendaji kutokana na utendaji usioridhisha. Baadhi ya watendaji walioondolewa katika siku za mwanzo ni pamoja na aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rished Bade, aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco) Mhandisi Benhadard Tito. Mbali ya uwajibikaji, Rais Magufuli amefanikiwa kupambana na mzimu wa wafanyakazi hewa, akiwabaini na kuwaondoa 19,629 hivyo kuokoa kiasi cha Sh19.7 bilioni zilizokuwa zikilipwa kwa mwezi. Mbali na wafanyakazi hewa, Serikali pia imechuja wanafunzi hewa wa elimu ya juu waliokuwa wakipata mikopo na kuisababishia Serikali hasara.