Kauli ya minziro hii hapa

http://maisharaisi.blogspot.com/2017/03/kauli-ya-minziro-hii-hapa.html
Benchi la ufundi la Singida United limeanza kuwafuatilia kimyakimya baadhi ya nyota wa timu za Ligi Kuu huku likisisitiza kutosajili wachezaji mizigo kwa ajili ya msimu ujao wa ligi. Timu hiyo inayonolewa na kocha. Fred Felix Minziro ni miongoni mwa klabu tatu zilizopanda Ligi Kuu msimu ujao sambamba na Njombe Mji ya Njombe na Lipuli ya Iringa. Kocha Minziro alisema kuwa amejipanga kuzunguka katika viwanja mbalimbali nchini kutazama mechi zilizosalia za Ligi Kuu ili aone wachezaji gani wanaweza kuimarisha kikosi chake msimu ujao. "Kwa sasa siwezi kusema ni wachezaji wangapi hasa nitawasajili kwani muda bado upo wa kutosha kukutana na viongozi wangu na kujipanga, lakini tayari nilishaanza kuwafuatilia baadhi ya wachezaji kimyakimya kabla hata ligi daraja kwanza haijaisha. Kocha huyo alitamba kuwa hataki Singida United iwe jalala la kuhifadhia wachezaji waliokuwa mzigo kwenye timu nyingine. "Wachezaji nitakaowachukua ni wale ambao nimejiridhisha hasa kuwa wana ubora na uwezo wa hali ya juu kuitumikia timu. Wale ambao wametemwa kwenye timu zao kisa uwezo wao uko chini wasitarajie kuwa nitawasajili. Sitaki kuwa na wachezaji wa kukaa benchi tu," alitamba Minziro.