Madudu yaliyojificha Stendi ya Mabasi Mbeya


Harakati katika stendi kuu ya mabasi mjini

Harakati katika stendi kuu ya mabasi mjini Mbeya.Jengo linalooneka ndilo ambalo wahuni wamejimilikisha na kudai kodi ya pango kwa abiria wanaolala baada ya mabasi kuchelewa .Picha na mpigapichawetu 
Mbeya. Wakati wasafiri wanaofika usiku Stendi Kuu ya Mabasi Mbeya wakitarajia kujihifadhi kwa usalama kwenye jengo lililopo, imegundulika kuwa kuna vitendo vya ukiukwaji wa maadili vinavyoendelea ikiwamo ubakaji, uporaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Stendi Kuu ya Mabasi ya Mbeya iliyopo Kata ya Sisimba imekuwa kama dimbwi lililojaa kila aina ya uchafu, hususani nyakati za usiku.
Waandishi wa habari waliofanya uchunguzi kwa siku mbili wakati wa mchana na usiku walishuhudia uvutaji wa bangi ukishamiri nyuma ya kituo hicho karibu na mto. Kadhalika nyakati za usiku wapo vijana waliojimilikisha sakafu yote ya jengo la stendi ambao kazi yao ni kuwatoza fedha wasafiri wanaofika usiku na kutaka kujipumzisha katika eneo hilo.
Miongoni mwao, vijana wawili wanatajwa zaidi kwamba wanaendesha vitendo vya ulawiti kwa abiria wakiwamo wanafunzi wanaolala stendi hapo kwa ajili ya safari za kesho pamoja na wale wanaofika usiku katika eneo hilo.
Uchunguzi wa waandishi uligundua kwamba pamoja na kuwapo kituo cha polisi eneo hilo, lakini hakina msaada kwa abiria kwa vile kinafungwa saa 12.00 jioni hadi kesho yake saa 1.00 asubuhi na kutoa mwanya kwa wahuni kufanya vitendo vyao.
“Pamoja na kwamba polisi wanakifunga kituo hiki kwa kufuli, lakini wahuni mara kadhaa wanavunja kufuli na kulala ndani ya kituo hicho kuanzia saa 5.00 usiku na wanatoka humo saa 11.00 alfajiri kabla ya polisi kufika,’’ anasema muuzaji wa vinywaji kwenye ‘grocery’ moja inayotoa huduma zake kituoni hapo hadi usiku wa manane.
‘’Yaani dada (mwandishi) we acha tu hata sisi hapa wauzaji huwa tunayaona baadhi ya matendo yanayofanyika usiku, lakini ndiyo hivyo tunashindwa jinsi ya kuwasaidia hawa abiria kwani ukijaribu kuongea tu hawa vijana wanakwambia kaa kimya umefuata biashara na siyo umbea,’’anasema.
Anasema kama stendi hiyo ingekuwa na ulinzi wa polisi kwa saa 24, wahuni wangekosa mwanya wa kufanya yote hayo hususani nyakati za usiku.
Akizungumzia vituko vinavyofanywa stendi kuu, muuzaji wa tiketi za mabasi aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Kagile anasema wapo watu waliojimilikisha stendi hiyo na kuitaja kama ni mali ya Mombasa.
Kagile anasema kipindi cha kufungua ama kufunga shule, matukio ya ulawiti kwa watoto yanakuwa mengi huku wasafiri wengine wakilalamikia kuibiwa fedha.
Anasema: “Matukio hayo yote yanatokea kwa abiria ambao wanakata tiketi kwenye mabasi ambayo hayapo na wengi wanarubuniwa na kujikuta wakihangaika hata siku mbili.” anasema.
Naye muuzaji wa mgahawa aliyejitambulisha kwa jina la Monica Mwatipulo anasema jengo la stendi kuu nyakati za usiku linamilikiwa na mtu mmoja ambaye anatandika makaratasi magumu chini na kuwapangisha abiria wanaotaka kulala.
Anasema kwa ujanja wake anatandika makaratasi hayo kwenye maeneo ambayo hayavuji wakati wa mvua, lakini kwa watu wasio na fedha anawaelekeza walale maeneo yanayovuja.
‘’Wakati mwingine anaweza akatoa adhabu kwa abiria ambaye ndiyo mara yake ya kwanza kufika stendi hapa na yule asiye na fedha kwa kuwaambia waondoke kabisa ndani ya jengo hilo na hii inatokea wakati akiwa na wateja wengi,’’anasema.
Abiria wakodishwa maboksi ya kulalia
Waandishi waliojifanya ni abiria walipofika eneo hilo usiku waliwakuta watu kadhaa wakiwa wamelala kwenye makaratasi ya kaki na wengi wakiwa wamekaa tu pembezoni mwa jengo hilo ambapo wale waliolala walisema walilipia kati ya Sh500 na Sh2,000 kutegemea ukubwa wa karatasi.
‘’Nimemlipa kaka mmoja wanamwita Mombasa Sh1,500, na sasa ameondoka ila kama unataka kulala msubirie anaweza kurudi sasa hivi ili nawe umlipe, ’’ anasema abiria wa kike aliyejitambulisha kwa jina na Hanariel Kaniki aliyefika saa 5.00 usiku akitokea Tabora na alikuwa akielekea Ileje.
Hanariel anasema mwanaume huyo aliwatangazia abiria waziwazi kwamba yeye ndiye anayepokea wageni wa usiku wa manane, hivyo wanaotaka kulala hadi kesho yake wachague maeneo ya kulala kwa vile mabasi mengine yalikuwa njiani na kwamba nafasi zitajaa haraka na kupelekea wengine kukosa sehemu za kulala.
Wakati waandishi wakiyashangaa hayo, anajitokeza muuza mgahawa aliyejitambulisha kwa jina la Sekela Amoni ambaye anasema yeye mara nyingi huwa anafika stendi hapo saa 10:45 alfajiri na kuwakuta abiria wengi kwenye jengo hilo wakiwa bado wamelala, lakini ikifika muda wa mabasi kuanza safari hapo ndipo anajitokeza kaka huyo (Mombasa) anayakusanya maboksi yake na kwenda nayo anakojua yeye.
Kwa mujibu wa Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Denis Daud, stendi kuu hiyo inapitiwa na wastani wa mabasi 45 kwa siku.
Mara kadhaa mabasi yanayofika jijini hapa nyakati za usiku ni yale yanayotoka Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Zimbabwe, Zambia na DRC Congo.
Abiria mwingine aliyelala eneo hilo na kujitambulisha kwa jina la Maganga Nkunambele anasema alilipia Sh2,000 kwa kulala pale na kwamba alimkabidhi fedha hizo mwanamme aliyetangaza kwamba eneo hilo ni lake.
Uporaji pochi
Madudu mengine kwenye kituo hicho cha mabasi ni uporaji ambao unadaiwa umekithiri hususan kwenye vichochoro vya kuingilia katika eneo hilo.
Muuzaji wa tiketi aliyejitambulisha kwa jina la Ally Mustafa anasema wastani wa matukio matatu ya wanawake kuporwa yanatokea nyuma ya kituo cha mabasi karibu na kijito ambacho kimegeuzwa makazi ya vibaka na wavuta bangi.
Mama lishe ambaye jina lake linahifadhiwa anasema suala la wavuta bangi na wabwia unga linajulikana waziwazi kwa viongozi na kwamba hata baadhi ya polisi wanashiriki.
“Hata polisi anayeitwa (Jina linahifadhiwa) anashiriki kwenye vitendo vya kuvuta bangi,’’ anasema.
Stendi kuu ya mabasi ipo karibu na ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sisimba ambayo ilidaiwa kupokea malalamiko na kutoyafanyia kazi.
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Furaha Malele alipoulizwa kuhusu madudu ya stendi kuu, alisema yalisharipotiwa polisi siku za nyuma huku akisisitiza kwamba yeye siyo msemaji.
Uongozi wa jiji washangaa
Uongozi wa jiji ulipoulizwa kuhusu madudu kwenye stendi hiyo, yakiwamo ya watu kujimilikisha sakafu ya jengo la stendi ulisema hauna taarifa .
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi, Ofisa Habari wa Jiji, John Kilua, alisema hawakuwa na taarifa zozote kuhusu madudu hayo na kwamba watayafanyia kazi malalamiko hayo ili kujua kinachoendelea.
Kuhusu vitendo vya ulawiti na uporaji, alisema kwa kawaida stendi hiyo ipo chini ya ulinzi wa polisi na ndiyo wanaofanya doria za mara kwa mara hata nyakati za usiku.
Msako wa kushtukiza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari alipoulizwa kuhusu matukio mabaya katika kituo hicho, alisema ni kweli yapo na polisi wamekuwa wakifanya msako wa kushtukiza mara kwa mara.
Kuhusu baadhi ya polisi wake kushiriki kwenye uvutaji wa bangi na dawa za kulevya, Kamanda Kidavashari alisema taarifa hizo atazifanyia kazi.



Related

kitaifa 3574748929495407534

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii