Lissu: Tumeshinda, tumeshashinda






“Tumeshinda. Tumeshashinda.” Hayo ni maneno aliyoyatamka Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akimweleza Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe aliyekwenda kumjulia hali jijini Nairobi, Kenya.
Lissu ambaye ni mwanasheria wa Chadema ametimiza siku 13 tangu alazwe katika Hospitali ya Nairobi (Nairobi Hospital) na hali yake inaendelea vizuri baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7, nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.
Baada ya kumuona Lissu, Zitto ambaye ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo alitumia mitandao ya kijamii hasa ukurasa wa Facebook kuandika kwa kuanza na kichwa cha habari ‘Ujasiri’ kisha akaendelea kuandika, “Nimetumia wikiendi iliyopita kumsabahi ndugu Lissu Nairobi. Nimerudi nikiwa mwenye unyenyekevu zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri ambao kaka yangu ameuonyesha licha ya kuwa yupo kwenye maumivu makali.”
“Si mara nyingi hapa nchini utasikia tukiongelea ujasiri. Lakini namfikiria Lissu na vile nilivyojisikia nikiwa pamoja naye Nairobi. Najua hivyo ndivyo alivyo. Waliomshambulia wamemuumiza. Wamemuumiza kweli. Na bado wakati tuliokuwa naye amenionyesha shukrani, ari na ucheshi. Huo ni ujasiri.”
Zitto aliendelea kwa kuandika kuwa, “alichopitia na anachoendelea kupitia Lissu siyo kitu rahisi kwa mtu yeyote, kutafakari na kufikiria hali ile kungeniacha nimeumia moyo kama asingesema maneno haya kwangu: ‘Tumeshinda Tumeshashinda’.”
Mbunge huyo alimalizia kwa kuandika, “ujasiri ni Lissu.”
Wakati Zitto akiandika hayo, juzi wabunge na meya wa Chadema walifanya ibada ya kumuombea Lissu iliyofanyika jijini Nairobi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri. Waliohudhuria ibada hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, John Heche (Tarime Vijijini), Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita.
Baada ya kumalizika ibada hiyo, Mchungaji Msigwa aliwashukuru wote walioonyesha mapenzi mema kwa Lissu na kwa Chadema na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kumuombea mwanasiasa huyo na kutoa michango.
Wakati Mchungaji Msigwa akieleza hayo, Lema alisema wakati huu umekuwa wa hofu, hivyo aliwasihi watu wote wa Afrika Mashariki kumuomba Mungu aiondoe akigusia pia uchaguzi Mkuu wa Kenya.

Related

kimataifa 4029741254755386492

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii