Bombardier iliyozuiwa Canada yaja

    


Hatimaye ndege aina ya Bombardier Q400 iliyokuwa imezuiwa Canada kwa zaidi ya miezi minane inatarajiwa kutua katika ardhi ya Tanzania wakati wowote kuanzia sasa.
Ndege hiyo, ambayo ni ya tatu kununuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, ilikuwa iwasili nchini Julai mwaka jana lakini ilizuiliwa ikidaiwa kwamba ni kutokana na Serikali kudaiwa Dola za Marekani milioni 38, (zaidi ya Sh87 bilioni) na kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd ya Montreal, Canada.
Hata hivyo, haijafahamika kama Serikali imelipa deni hilo au imeshinda kesi iliyokuwa imefunguliwa katika Mahakama Canada.
Jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa kupitia ukurasa wake wa Twitter aliweka picha ya ndege hiyo na ujumbe ukisomeka, “Ndege yetu aina ya Bombardier Q400 iliyokuwa imezuiwa nchini Canada ilikwishaondoka Canada kuja Tanzania.”
Msigwa aliongeza, “Aidha, ndege kubwa nyingine 3 (2 Bombardier CS300 kutoka Canada & 1 Boeing 787-8 Dreamliner kutoka Marekani) zitawasili baadaye mwaka huu. Nawatakia Ijumaa Kuu njema.”
Alipopigiwa simu, Msigwa alifafanua kwa ufupi kuwa ndege hiyo ilitakiwa kufika nchini mwaka jana lakini ilishindikana kutokana na sababu mbalimbali.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, alipoulizwa muda ambao ndege hiyo itawasili nchini alisema; “Imeondoka Canada iko njiani inakuja. Tunaendelea kufanya mawasiliano na kuhusu itafika lini, ukinipigia kesho (leo) nitakuwa katika nafasi nzuri ya kukujibu.”
Alipoulizwa kuhusu deni hilo kama limelipwa au utaratibu upi umetumika hadi kuachiwa, Nditiye alisema, “Kuna taratibu za kimahakama zilikuwa zinaendelea, hayo tutapata taarifa zake kwa kina ikishafika na tutakuwa na nafasi ya kutoa taarifa kwa umma.”
Kukwama kwa ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 75 kuliibuliwa na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Agosti 17 mwaka jana.
Lissu alisema ndege hiyo ilikamatwa baada ya kampuni hiyo ya ujenzi kuishtaki Serikali, ikipinga kuvunjiwa mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo, jijini Dar es Salaam mwaka 2003.
Hata hivyo, baada ya Lissu kutoa madai hayo, Serikali ilitoa ufafanuzi ikikiri kuwapo kwa mgogoro uliosababisha ndege hiyo kukwama huku akisema imeanza njia za kidiplomasia kulimazima.
Agosti 19 mwaka jana, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa aliwaambia waandishi wa habari kwamba kuna mgogoro ambao kimsingi ulisababishwa na wanasiasa.
“Ndege zinazonunuliwa ikiwepo hii ambayo imetengenezewa mizengwe na hao Watanzania wenzetu. Sio ya Rais (John) Magufuli, bali ni za Watanzania wote. Hawa baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaoshabikia migogoro inayokumba jitihada za Rais wetu za kutuletea maendeleo, hawana uzalendo,” alisema.
Pia, alizungumzia kuwapo kwa kesi mahakamani huko Canada lakini hakufafanua undani wake.
Novemba 7 mwaka jana, Rais Magufuli alipokuwa akizindua Uwanja wa ndege mjini Bukoba mkoani Kagera, alizungumzia sakata hilo na kusema amemwandikia barua Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau akimtaka ashughulikie kwa haraka suala hilo.
Alisema licha ya kuandika barua hiyo, alimtuma Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda huko kushughulikia suala hilo kisheria.
“Nimemwandikia barua waziri wa Canada kuulizia ni kwa nini ndege yetu inakaa zaidi ya miezi sita... pia nimemtuma mwanasheria akapambane kisheria,” alisema Rais Magufuli.
Akitoa sababu za kukamatwa kwa ndege hiyo, Lissu alisema; “Kabla ya kukamilisha zabuni hiyo mkataba ulivunjwa na katika mazingira ya ajabu yaani kuvunja mikataba kwa kukurupuka na bila kuzingatia sheria. Kampuni hiyo ilinyang’anywa kandarasi hiyo na kutimuliwa nchini. Stirling Civil Engineering Ltd. ikafungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi.”
Alisema Desemba 10, 2009 na baadaye Juni 10, 2010 Mahakama ya Usuluhishi ilitoa tuzo ya takriban dola za Marekani milioni 25 pamoja na riba hadi malipo kamili yatakapofanyika.
Lissu alisema tuzo hiyo imesajiliwa na kutambuliwa kama deni halali la Serikali ya Tanzania kwa Stirling Civil Engineering Ltd. katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Uingereza na Uganda.
“Licha ya jitihada mbalimbali za kulipwa deni lake, hadi sasa Serikali ya Tanzania haijalipa deni hilo ambalo sasa, kwa sababu ya ucheleweshaji wa malipo, limeongezeka hadi kufikia dola za Marekani 38,711,479 kufikia Juni 30, 2017. Hapo ndipo Stirling Civil Engineering Ltd. ilipoamua kuomba amri ya Mahakama Kuu ya Montreal ya kukamata mali zote za Tanzania zilizopo Kampuni ya Bombardier, zikijumuisha ndege ya Bombardier Q400,” alisema Lissu.
Mwaka 1999 Serikali iliipa kandarasi kampuni ya Impresa Ing. Fortunato Federici SpA (IFF) ambayo baadaye ilinunuliwa na Stirling, kukarabati barabara ya Wazo Hill-Bagamoyo, lakini baadaye ikatimuliwa.
Mwaka 2004 kampuni hiyo ilifungua kesi Mahakama ya Usuluhishi wa Kimataifa na hukumu ilitolewa mwaka 2009 na 2010, lakini Serikali haikulipa fidia.
iliyopendekezwa na kuilazimu kukazia hukumu Uingereza na Uholanzi.
Novemba 2015, mahakama nchini Uingereza iliridhia utekelezaji wa hukumu hiyo na Uholanzi ilifanya hivyo Desemba 2016.

Related

kitaifa 7447529566705252081

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii