‘Msichague watakaowafanya muishi kwa kuogopaogopa’

http://maisharaisi.blogspot.com/2018/03/msichague-watakaowafanya-hi-kwa.html

Waamini wakatoliki wakiwa wamepanga mstari kubusu Msalaba wakati wa Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mhashamu Askofu Evarist Chengula alipokuwa akiongoza ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria wa Fatma, Mwanjelwa jijini Mbeya na kuonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Taifa (TBC1).
Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Chengula alisema ujumbe uliotolewa na maaskofu siku kadhaa zilizopita ulikuwa haumlengi mtu fulani, bali wanafiki wanaodai ni Wakristo, lakini hawana imani ya dini hiyo ili waweze kubadilika na kuwa watu wema.
“Tuangalie, kulialia tu hakuna maana. Tufikiri kabla ya utendaji kitu, sisi maaskofu tumeona udhaifu wetu ni huu, kila mara baada ya uchaguzi ndiyo tunaanza kumu – analyse (chambua) mtu, kumtathmini mtu kwamba ataweza au hawezi.
“Hakuna maana tufurahie watu fulani tumewachagua, lakini tunaishi katika hali ya wogawoga, sasa wote tunaanza uchaguzi wa mwaka kesho,” alisema.
Aliwataka waumini kupitia jumuiya ndogondogo waanze kufikiri mwaka ujao watamchagua nani, “Mnielewe vizuri, si chama fulani, watu walio na tabia fulani. Tunataka nini, tunataka maendeleo, tunataka amani, tunataka watu tutendeane haki, lazima katika jumuiya ndogondogo tuwe tayari, tumeonyesha kifikra kwamba watu wa namna hii wapo katika jamii zetu.
“Pale watakapokuja kujiandikisha kwamba wanataka kupigiwa kura ya udiwani au uongozi wa vitongoji, tuwe tunajua kwamba tunamchagua mtu wa aina gani. Ujumbe wa mwaka huu tunasema hakuna maana kusikiliza kila kitu tu, badala yake tufikiri kabla ya kutenda.”
Askofu Chengula alifafanua kwamba kauli yake hiyo haimaanishi kwamba sasa ni wakati wa kuchagua chama fulani kwani wakifanya hivyo wataingia katika shimo lilelile, kwani watachagua mawazo ya watu fulani. “Je, wakiwapatia watu wasioendana na matarajio yenu mtasema nini?
“Tunafikiria yetu, tunataka chama fulani ndio kiongoze, ndio kitutendee sisi badala ya kufikiri waliochaguliwa wawe na lengo moja tu, kutufanya tupate haki zetu sisi Watanzania na kuishi kwa amani.”
Aliwataka waumini wajitathmini wao nani, wanataka mtu wa aina gani, “ili hata sisi tuweze kutimiza azimio la Umoja wa Mataifa walilofanya miaka 70 iliyopita kwamba lazima kila mmoja aishi akipatiwa haki akitendewa haki na mwisho kuwe na amani.”
“Wanangu sisi hatuna ubaya na mtu yeyote, ujumbe ule tumeutoa kwa kujiangalia wote, tuanze kujiandaa mwaka 2019 tuchague watu, tunaweza kukosea kwa sababu binadamu hana ukamilifu wa kufikiri, lakini kwa vyovyote vile hatutawatupia lawama watu wengine kwa sababu tumejitahidi kadri ya uwezo wetu...” alisema.
Alimtaka kila mmoja akitoka kanisani hapo aende akasimulie anakokwenda kwa sababu ni vita ya wote, kwa sababu wakipata viongozi wabaya wataumia wote na wakipata wazuri watafaidika wote na kila mmoja aone kiu kuona Tanzania yenye upendo.
“Kila anayekuja kubusu msalaba huu tulioulaza hapo mbele, amueleze Yesu nataka Tanzania yenye upendo,” alisema Askofu Chengula.
Wahimiza amani
Mbali ya Mbeya ambako ibada hiyo ilifanyika kitaifa, kwingineko nchini viongozi wa Kikristo wamehimiza amani, upendo na kusameheana wanapoadhimisha mateso ya Yesu Kristo. Wamehubiri umuhimu wa kuepuka makundi na kuombea amani ya nchi.
Akihubiri katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam, Padri Baitu Juvenalis, aliwataka Wakristo kukumbuka mateso ya Yesu kwa kudumisha amani na kusameheana.
“Yesu aliteswa bila hatia, lakini alisamehe na kuonyesha wema na upole na ndio maana aliyapokea yote hata yaliyokuwa ya dhuluma,” alisema Padri Juvenalis na kuongeza:
“Yesu aliteswa ili kutukomboa, tunapaswa kutoa shukurani kwa matendo na si maneno. Tunapaswa kuonyesha upendo, kusamehe na kutoweka visasi, tufanye kwa ajili ya Ukristo wetu.
Padri Juvenalis akihubiri katika ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo alisema Yesu ameteswa na anawakumbusha waumini kuteswa kwa ajili ya haki.
“Ukweli wa Mungu unaeleweka, hata wakisema sivyo na wakaandika sivyo lakini ukweli wa Mungu utabaki pale pale.”
Alisema Wakristo hawana budi kuonyesha unyenyekevu kwa kutembea huku wakijiamini. “Na kama unachokifanya ni cha kweli kwa nini utetemeke.”
Alisema viongozi wa dini wapo tayari kuzungumza mambo ya imani na si yale yaliyotokea hapa na pale.
“Tukuze Ukristo wetu kwa kutenda yaliyo mema ili tuweze kumtangaza Kristo. Tukumbuke kupiga magoti na kuomba Mungu hata katika hoja tunazochangia,” alisema.
Nje ya kanisa, paroko msaidizi wa kanisa hilo, Padri Venance Tegete alisema shetani anaweza kuja kwa njia mbalimbali, “Hivyo tunapaswa kudumisha amani, kuvumiliana na kupendana.
Katika ibada hiyo iliyofanya kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Azania Front jijini Dar es Salaam, Askofu Alex Malasusa aliwataka Wakristo kutokuwa watu wa makundi na badala yake kuishi maisha yanayompendeza Kristo.
Dk Malasusa, ambaye ni Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Mashariki na Pwani aliwataka Wakristo kupambana katika vita ya mabaya wanayokutana nayo kwa kutenda yaliyo mema.
“Hakuna sababu ya Wakristo kuendelelea kunyong’onyea na badala yake kumkabidhi Kristo maisha ya hapa duniani,” alisema.
Katika ibada hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam, Padri Aszi Mendonca alisema kifo cha Yesu ni ishara ya ukombozi kwa wanadamu hivyo ulimwengu bila msalaba usingekuwa wa matumaini.
“Nawaomba waumini kuitumia siku hii kutafakari maumivu ya Yesu yaliyofanya ukombozi kwao kwa kufanya mema,” alisema Padri Mendonca
Askofu Mteule wa Jimbo Kuu la Arusha, Isaac Amani akihubiri katika hiyo iliyofanyika katika Jimbo Kuu Katoliki, Kristo Mfalme aliwataka waumini kuomba bila kuchoka katika kipindi hiki cha kusubiri kufufuka kwa Yesu Kristo.
“Tumtumikie Mungu bila kuchoka na hiyo ndiyo fahari yetu kwa Mungu. Tumwombe Mungu atusimamie kwenye shughuli zetu kwa upendo wa ajabu huku tukiendelea kutafakari zawadi alizotujalia,” alisema.
Imeandikwa na Kalunde Jamal, Pamela Chilongola, Ibrahim Yamola, Janeth Joseph, Kelvin Matandiko na Godfrey Kahango.