MTANZANIA ALIYEMUUA MKEWE APANDISHWA KIZIMBANI UINGEREZA

Salum (38) anadaiwa kumuua mke wake, Leyla, Ijumaa ya wiki iliyopita kwa kumchoma visu mara kadhaa shingoni na kifuani. Mauaji hayo yalifanyika nyumbani kwa wanandoa hao, Kirkstall Avenue, Haringey, Uingereza.
 Leyla, ni mtoto wa Hidaya Mtumwa, mwanamke aliyewahi kutungiwa wimbo na mwanamuziki wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Pepe Kale, miaka ya 90.
Hata hivyo, kesi ya Salum haikuweza kusikilizwa baada ya kuwepo kwa mgomo wa wanasheria wa ngazi za juu nchini humo ulioanza tangu Aprili Mosi, mwaka huu.
Wakili wake, Seona White amesema amewasiliana na vitengo zaidi ya 20 vya wanasheria, lakini hakuna aliyekubali kumtetea Salum kutokana na mgomo unaoendelea.
“Sijui hali hii itaendelea kwa muda gani lakini natumaini mgogoro utatatuliwa haraka,” amesema.
Jaji wa mahakama hiyo, Anuja Dhir amesema kesi hiyo itasikilizwa tena Juni 20 na akaamuru mtuhumiwa arudishwe mahabusu.
Jaji Dhir amesema mbele ya mahakama hiyo kuwa, licha ya Salum kukosa wakili wa kumtetea mahakamani, lakini mwanasheria wake hana budi kuhakikisha anapata haki zake msingi kwani si makosa yake.
Salum alitafsiriwa lugha ya Kiingereza na mkalimani  mahakamani hapo.

Related

kimataifa 3539338024779419581

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii