Rais Magufuli aigomea PSPF


Rais  John  Magufuli  akipokea Zawadi ya picha

Rais John Magufuli amekataa ombi la Mfuko wa Pensheni wa PSPF kufuta viwanja viwili vinavyomilikiwa na ubalozi wa Zimbambwe na Wizara ya Kazi na Ajira ili kulinda mandhari ya jengo lake jipya.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo alipozindua jengo la ghorofa 11 la PSPF na tawi la Benki ya NMB lililopo Chimwaga mjini hapa.
Awali, mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo, Mussa Iyombe alimuomba Rais kuvifuta viwanja hivyo ili kulinda mandhari ya jengo hilo kwa ajili ya eneo hilo kutumika kuegeshea magari ya wateja wa jengo lao.
Iyombe, ambaye pia ni katibu mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), alisema Rais alishatoa maelekezo kwa mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuwa mabalozi pamoja na wizara watapewa viwanja vingine.
“Sasa uwepo wa viwanja hivi hapo mbele ya jengo hili unapunguza mandhari yote ya jengo hili zuri kwa Mkoa wa Dodoma. Kwa sababu wewe ndio mamlaka najua huwezi kutuacha hivihivi. Kwa heshima na taadhima, kwa niaba ya bodi ya wadhamini tunakuomba mheshimiwa Rais ufute hati zile za viwanja viwili ili eneo hilo libaki kama sehemu ya maegesho kwa wateja wetu,” alisema.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema hatafuta hati za viwanja hivyo kwa sababu eneo kwa ajili ya maegesho walilonalo PSPF linatosha kwa magari zaidi ya 100 na hata michoro ya majengo ya wamiliki wa viwanja hivyo bado hawajayaona.
“Kwa hiyo hili mimi sitalifanya, ninataka nizungumze hapa kwa uwazi kabisa kwamba suala la kufuta halipo kabisa. Kwamba suala la kufuta viwanja ambavyo vipo karibu na vingine, ikiwa hivyo na Ikulu nyumba zote zinazozunguka ningekuwa nimezifuta,” alisema.
Alisema wao (Ikulu) wanakaa na wananchi ambao ni majirani na huo ndio utanzania na kuwataka PSPF kama wanataka kuwaondoa wamiliki wa viwanja hivyo wazungumze nao.
“Muwanunue ili muweze kujenga majengo mnayoyataka yapendezeshe mazingira mnayotaka. Lakini la kutumia madaraka yangu kufuta viwanja ambavyo havina makosa, ambavyo waliomba kwa mujibu wa sheria siwezi nikaingilia,” alisema.
Akizungumzia gawio kutoka Benki ya NMB, Rais Magufuli alitaka watu wanaofanya kazi kwa niaba ya Serikali kuangalia ni kwa nini gawio linalotokana na hisa za Serikali katika benki hiyo haliongezeki kwa miaka mitatu mfululizo.
Alisema amesikitishwa kwa gawio hilo kubaki kuwa Sh16.5 bilioni kwa miaka mitatu mfululizo.
Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Eneke Bussemaker alisema benki hiyo katika kipindi cha mwaka jana ilitoa Sh1 bilioni kwenye faida yake kununua madawati 6,000, kompyuta na vitanda kwa ajili ya hospitali kadhaa nchini.

Related

kitaifa 1690257784723315924

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii