Serengeti Boys yabebeshwa mzigo wa 2019



Mashabiki wa soka wa Tanzania wakifuatilia moja
Mashabiki wa soka wa Tanzania wakifuatilia moja ya michezo ya timu ya vijana ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Picha ya Maktaba 

 Wakati Fainali za Mataifa ya Afrika Afcon 2017 zikimalizika kwa Cameroon kutwaa ubingwa kwa kuilaza Misri mabao 2-1, timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’ imetajwa kama kimbilio pekee linaloweza kuifanya Tanzania ifuzu fainali hizo.
Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kuanza harakati zake za kufuzu fainali hizo Cameroon mwaka 2019, na timu pekee ya kuipeleka huko ni Serengeti Boys.
Wakitoa maoni yao juu ya fainali hizo zilizomalizika juzi, wadau mbalimbali wa soka waliliambia gazeti hili kuwa maandalizi mazuri kwa Serengeti Boys ndiyo yatakayotengeneza Taifa Stars kwa ajili ya Afcon miaka ijayo.
“Cameroon na Misri wametupa fundisho kuwa hakuna kinachoshindikana kama kumefanyika uwekezaji wa soka la vijana.
Kauli za wadau
Vijana waliozifikisha fainali timu hizo wote wameonyesha kiwango cha juu licha ya kutokuwa na majina makubwa. Kikubwa kwetu tunachopaswa kufanya ni kuweka msisitizo kwa Serengeti Boys kwa kuipa maandalizi mazuri ya kuwafanya vijana wawe fiti kimbinu na kimwili ili miaka kadhaa ijayo wao ndio wawe wachezaji wa Taifa Stars,” alisema kocha wa Mwadui, Ally Bushiri.
Mbunge wa Jimbo la Malindi, Ally Salehe ambaye ni wakala wa kimataifa wa soka, alisema kuwa mkazo iwe ni kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kuanzia mwaka 2021 na sio 2019.
“Hakuna nchi inaweza kufanikiwa bila kuandaa msingi mzuri ambao ni kuwa na timu imara za vijana kwa nchi na klabu.
“Kwa kuwa tayari timu yetu ya taifa ya vijana imefuzu fainali za Afrika, ni vyema sasa kuhakikisha hiyo inaendelezwa ili ndio ije kuwa timu ya taifa baadaye katika fainali zitakazofuata na sio hiyo itakayofanyika Cameroon. Naamini hakuna kinachoshindikana,” alisema Salehe.
Kipa wa zamani wa Taifa Stars, Ivo Mapunda alisema kuwa Serengeti Boys ndio msingi imara wa timu ya taifa kwa siku za usoni.
“Tunatakiwa kuwa na mipango endelevu na kujifunza kutokana na wenzetu. Lazima wachezaji waandaliwe mapema tangu wakiwa wadogo na kupewa misingi ya soka ambayo ndiyo msingi mkuu wa kujenga timu imara ya taifa.
Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ambaye alikuwemo katika kikosi cha Stars kilichofuzu Afcon mwaka 1980 , alisema kinachotakiwa ni kujipanga vizuri na kupata mechi za maana.
“Kwanza inabidi tupate profesheni wengi yaani wachezaji wengi waende kucheza soka la kulipwa nje ili kupata vitu vya ziada,” alisema.
Mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema kuna vitu vingi ambavyo wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kujifunza, lakini kubwa ni kujituma kwa asilimia 100.
“Fainali za Afcon 2017 ziwafungue wachezaji wa Tanzania. Ninaimani wameona jinsi wenzao walivyokuwa wakicheza kwa kujituma, na katika hali ya kujitoa muhanga,” alisema Mogella.
Beki na kiungo wa zamani wa Taifa Stars, Mohamed Rishard Adolf alisema tatizo kubwa linalotuangusha Watanzania ni kuchukulia vitu kirahisi rahisi.
“Kwa mfano, ukiangalia Fainali za Afcon mwaka huu, kwa jinsi tulivyoona, inabidi yatufunguea macho na kuiangalia upya ligi yetu, tuangalie ubora wa wachezaji wetu, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na pia ari ya kupambana. Tumeona watu walivyokuwa wakipambana unaona kweli hapa soka imepigwa,” alisema.
Mshambuliaji wa Simba, Mohammed Ibrahim alisema timu nyingi zilizoshiriki fainali za mwaka huu zimeonekana kubebwa na wachezaji wengi wanaocheza soka nje ya mataifa yao jambo ambalo Tanzania itunalikosa.
“Mashindano ya mwaka huu yanavutia kwani timu nyingi zimeonekana kujiandaa na nyingine zimeshangaza kwa kupata matokeo yasiyotarajiwa.
“Ila nilichojifunza ni wachezaji wa Tanzania tunatakiwa kutoka wengi na kwenda kucheza soka nje ya nchi ili kuisaidia timu yetu ya taifa kwani ukiangalia timu nyingi zimebebwa na wachezaji ambao kwa sehemu kubwa hawachezi ligi ya mataifa yao,” alisema Mo Ibrahim.


Related

michezo na burudani 5844702044568819257

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii