Kingue arejea azam

http://maisharaisi.blogspot.com/2017/03/kingue-arejea-azam.html
Kikosi cha Azam kinachojiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland kimeongezewa nguvu baada ya kurejea kwa kiungo Stephane Kingue. Mchezaji huyo alikuwa nje ya uwanja tangu alipoumia nyama za paja kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba wiki tatu zilizopita. Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Idd, alisema timu imeshaanza maandalizi ya mchezo huo utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi. "Kocha amesema mechi zilizopita dhidi ya Mwadui, Stand na za kimataifa dhidi ya Mamelodi na Red Arrows zimemsaidia katika matayarisho ya kikosi chake,"alisema Idd. Hivi karibuni kocha wa Azam, Aristico Cioaba amesema changamoto inayoikabili timu yake ni kushindwa kuzitumia nafasi inazopata. "Unapocheza kwenye uwanja wa nyumbani lazima utumie nafasi, nataka timu icheze kwa kasi hasa inapofika eneo la adui. Ninafurahi wachezaji waliokuwa na majeraha wamerejea, inatuongezea hamasa wakati huu," alisema Mromani huyo aliyejiunga na Azam Januari mwaka huu. Mbali na Kingue, mshambuliaji John Bocco pia amerejea hivyo kukiongezea nguvu kikosi hicho.