Bodaboda wajengewa ofisi dar

Siku mbili baada ya mbunge wa Monduli, Julius Kalanga kuipinga halmashauri hiyo kuwatoza waendesha bodaboda ushuru wa Sh200 kwa siku, meya wa Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam ana mtazamo tofauti. Kalanga alipinga uamuzi huo katika kikao cha madiwani wa Monduli kuanzisha ushuru huo ambao waliupitisha na ulitarajiwa kuanza kutumika Julai mosi, akisema hatua hiyo inalenga kumtwisha mzigo dereva bodaboda ilhali kipato chake ni kidogo. Hata hivyo, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob amesema manispaa hiyo ina uwezo wa kukusanya mapato makubwa kutoka kwa madereva hao na wale wa bajaji endapo miundombinu katika maeneo ya vituo vyao yataboreshwa. Jacob alitoa kauli hiyo juzi wakati akizundua kituo cha pili cha ukusanyaji wa mapato cha manispaa hiyo kilichopo katika Kituo cha Daladala cha Simu 2000. Alisema miongoni mwa miundombinu inayotakiwa kuboreshwa ni wataalamu wa manispaa hiyo hasa wa mapato kuhakikisha wanawasajili na kuvipanga kwa namba vituo vya kazi vya madereva hao. Jacob ambaye ni diwani wa Ubungo (Chadema), alisema hatua ya baadhi ya bodaboda kutosajiliwa inasababisha kufukuzwa mara kwa mara na polisi na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), kwa madai ya kutowatambua. “ Ni wakati mwafaka kwa wataalamu wa Manispaa ya Ubungo kuwa wabunifu kwa kuumiza vichwa na kuhakikisha waendesha bajaji na bodaboda watambuliwa na kupangwa katika mfumo bora utakaowawezesha kulipa mapato,” alisema Jacob. Alisema kiwango kilichowekwa cha ushuru wa Sh 22,000 kwa mwaka wanacholipa bodaboda na zaidi ya Sh30,000 bajaji vikikusanywa kwa ufanisi manispa hiyo itapata mapato mengi yatakayoelekezwa kwenye uboreshaji wa maendeleo. Mhasibu wa Mapato wa Ubungo, Fulgence Luyagaza alisema kituo hicho kilikamilika mwezi Mei na ni mahususi kwa ajili ya kuwaondolea usumbufu wateja wanaolipa tozo mbalimbali.

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii