Lipuli, Ruvu hawana presha Yanga, Simba



 Pamoja na kupangwa kuanza Ligi Kuu Bara dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga klabu ya Lipuli iliyorejea baada ya miaka mingi hawana presha na mechi hiyo.
Benchi la ufundi la klabu hiyo linaloongozwa na Seleman Matola, umesema kuwa, wala hawajashtuka kupangwa na Yanga kwa sababu wanajivunia kikosi imara walichonacho, pia hata iweje ni lazima watetezi hao watakutana nao tu.
Matola alisema hana shida na upangwaji na ratiba kwa kuwa hata angeikwepa Yanga, mzunguko wa kwanza, angekuja kukumbana nao raundi ya pili, hivyo anachokifanya ni maandalizi ili kuhakikisha wanaanza kupata pointi tatu kutoka kwa mabingwa hao.
"Siwezi kubagua timu, najipanga kuona nafanya ushindani kwa kila mechi, hivyo kuanza na Yanga si kitu cha kunishitua, naandaa vijana wangu kupambana bila kujali timu watakayokutana nayo, hata kama inasifika kiasi gani, wao wanatakiwa kuonyesha uwezo na kuheshimu kazi yao," alisema
Naye Afisa Habari wa Ruvu Shoting, Masau Bwile kama ilivyo kawaida yake alieleza kwamba ni heshima kikosi chao kuanza na Simba, ili waweze kuwafukuzia msituni kwa madai kwamba hawastahili kukaa mjini.
"Ruvu siku zote tunajiamini, awamu hii tunataka kuzima kilele za usajili wa  klabu za Simba na Yanga ambao utadhani wamesajili Dunia, mwisho wa siku hatuoni wachezaji wao wakiwa na makali zaidi ya kutumia nguvu nyingi kupata matokeo," alisema.
Kocha msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor 'Cheche', alisema hawana wasiwasi wa ratiba hiyo, licha ya kukiri kwamba Ndanda ambayo wanafungua nayo dimba, imekuwa na ushindani mkali dhidi yao, lakini wanachukulia kama kipimo cha uwezo wao.
"Wakati mwingine ushindani tunaokumbana nao dhidi ya Ndanda, unatufanya kujituma ili kuonyesha taaluma zetu kujua tunakosea wapi hadi tupate ugumu wa kupata matokeo angali tunafanya usajili wa umakini," alisema
Naye kocha msaidizi wa Njombe Mji, Mrage Kabange, alisema wameifurahia ratiba kwani wanaanza kucheza nyumbani ambapo itawapa fursa mashabiki wao kuona mtanange huo dhidi ya Prisons.
Mechi ya pili watakutana na Yanga, kitu ambacho kocha huyo hakuonyesha wasiwasi zaidi ya kusema  wanawasubiri hao kina Donald Ngoma ili kuwaonyesha kazi na wazawa ambao hawana majina kama wao.
Kocha wa Prisons, Abdallah Mohamed, alisema ratiba ipo sawa, kikubwa wanajipanga kwa ajili ya kazi bila kujali wanakutana na nani.
"Ndiyo maana kuna muda ambao tunapewa kujiandaa, ratiba ipo sawa kwani lazima tutakutana na kila timu hivyo ni kujituma kuona tunapata matokeo," alisema Mohammed maarufu kama Bares.

Related

michezo na burudani 1759936616919511440

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii