Mtihani mgumu kwa Yanga CAF huu hapa


Wachezaji wa Yanga kutoka kushoto, Geofrey


Wakati droo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa kuchezeshwa kesho jijini Cairo, Misri, timu 10 zinaonekana tishio kwa wawakilishi wa Tanzania Yanga.
Yanga ni miongoni mwa timu 16 zilizofuzu hatua hiyo baada ya juzi kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 licha ya kufungwa bao 1-0 na Waleytta Dicha ya Ethiopia.
Timu hizo ni AS Vita Club kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), USM Alger (Algeria), Al-Hilal (Sudan), Enyimba (Nigeria), Asec Mimosas (Ivory Coast), CARA Brazzaville (Congo), Al-Masry (Misri), Djoliba (Mali), Raja Casablanca na RS Berkane za Morocco.
Uzoefu wa timu hizo katika mashindano ya kimataifa, mafanikio ambayo baadhi zimefikia na matokeo bora ambayo zimewahi kupata katika mechi zilizopita, yanaashiria wazi namna Yanga inavyoweza kukabiliana na shughuli pevu endapo itapangwa na miongoni mwa timu hizo kwenye kundi moja.
Wakati Enyimba, Raja Casablanca na CARA Brazaville zimewahi kutwaa ubingwa wa Afrika, USM Alger, Al-Hilal, ASEC Mimosas na Djoliba zimewahi ama kucheza hatua ya fainali au nusu fainali ya mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu.
Mafanikio ya timu hizo kumezifanya klabu hizo kuwa na uzoefu ambao mara kwa mara umekuwa ukizisaidia kufanya vizuri zinaposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho.
Ukiondoa miamba hiyo sita, Gor Mahia, Al-Masry na RS Berkane zimepata matokeo mazuri dhidi ya timu zilizoonekana ngumu na zenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa hatua inayotoa ishara kwamba siyo timu za kubeza kwenye mashindano hayo.
Al-Masry imefuzu baada ya kuzitoa Green Buffaloes ya Zambia, Simba ya Tanzania na CF Mounana ya Gabon.
Gor Mahia iliwatupa nje Supersport United waliocheza fainali mwaka jana wakati RS Berkane ilifuzu baada ya kuzitoa Mbour Petite-Côte (Senegal), Club Africain (Tunisia) na Generation Foot pia kutoka Senegal.
Droo itakavyochezeshwa
Timu itakayopangwa chungu cha kwanza itapewa uongozi wa kundi, ikifuatiwa na klabu kutoka chungu cha pili, pia kutakuwa na timu kutoka chungu cha tatu na nne.
Upangaji wa timu kwenye vyungu hivyo umetokana na pointi ambazo klabu husika imevuna kulingana na ushiriki na mafanikio kwenye mashindano ya Klabu Afrika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Yanga itawekwa chungu cha pili kutokana na kuwa na pointi mbili ambapo itakuwa na timu za Asec Mimosas, Williamsville za Ivory Coast na CARA Brazzaville ya Jamhuri ya Congo.
Chungu cha kwanza ambacho kitakuwa na timu nne ambazo kila moja itapewa uongozi wa kundi, kitakuwa na klabu za Al-Hilal, USM Alger, Enyimba na AS Vita Club.
Chungu cha tatu kitakuwa na timu za Al-Masry, Gor Mahia, Aduana Stars na Djoliba wakati chungu cha nne zimo RS Berkane, Raja Casablanca na Rayon Sports.
Yanga
Kutokana na utaratibu huo Yanga huenda ikajikuta inaangukia kundi lenye timu kutoka mataifa ya kiarabu kwa kuwa inaweza kupangwa na USM Alger au Al-Hilal zilizopo chungu cha kwanza, Al- Masry chungu cha tatu au mojawapo kati ya Raja Casablanca au RS Berkane zilizopo chungu cha nne.
Pia Yanga inaweza kuangukia kwenye kundi ambalo halina timu ngumu Enyimba, Gor Mahia na Rayon Sports ambazo zinaweza kuipa nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya robo fainali.
Kauli ya Mkwasa
Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa alisema wameandaa mpango mkakati wa kupata mafanikio katika hatua ya makundi.
“Tunachosubiri timu ifike kutoka Ethiopia, kila kitu kitajulikana, lakini kiutendaji tumeandaa mkakati madhubuti ambao siwezi kuweka wazi hadi timu itakapowasili,” alisema Mkwasa.
Pia alisema wamejipanga kiufundi na amewatoa hofu mashabiki wa Yanga kuwa timu hiyo itacheza kwa mafanikio.
Wasikie Pluijm, Julio
Kocha wa zamani wa Yanga ambaye aliiongoza timu hiyo kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2016, Hans van Pluijm alisema wawakilishi hao wa Tanzania wanapaswa kujipanga kikamilifu.
“Nawapongeza Yanga kufuzu hatua ya makundi wakiwa na hali waliyonayo sasa, sio kitu rahisi na wamefanya kazi kubwa inayostahili heshima lakini pia kufuzu kwao kuna faida kubwa kwa nchi.
Bado sijazifahamu timu nyingine zilizofuzu lakini kwa uzoefu wangu, hatua ya makundi ushindani unakuwa wa hali ya juu na unakutana na wapinzani wenye maandalizi na ubora mzuri, naamini Yanga watajipanga vizuri na watafika mbali,” alisema Pluijm.
Kocha wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema Yanga wanastahili kupongezwa kwa hatua waliyofikia, lakini wana kasoro mbili za kiufundi wanazotakiwa kuzifanyia kazi.
“Jambo la kwanza ambalo hata mimi mwenyewe nitajitahidi kulishauri benchi la ufundi la Yanga ni kuongeza programu za mazoezi ili wachezaji wawe fiti na stamina zao ziongezeke tofauti na sasa hawana nguvu jambo ambalo sio zuri pindi unaposhiriki hatua kama hii.
“La pili, wacheze kitimu bila kumtegemea mtu mmoja mmoja lakini pia ninafahamu kwamba kufanya vizuri zaidi kwa Yanga kunaweza kuisaidia nchi kuongeza idadi ya klabu kwenye mashindano ya kimataifa hivyo kwa hili walilofanya nawapongeza na nawaomba Watanzania wenzangu, tuiunge mkono Yanga ili iweze kufika mbali zaidi,” alisema Julio.

Related

michezo na burudani 7230323945038550422

Post a Comment

emo-but-icon

item
Kicbjamii